MAISHA YA SHULE YA SEKONDARI KIBAHA YACHANGIA KUIMARISHA UJUZI WA VITENDO KWA WANAFUNZI.
Kibaha, Septemba 2025
Katika kuendeleza elimu jumuishi na ya vitendo, Shule ya Sekondari Kibaha imekuwa mstari wa mbele katika kuwajengea wanafunzi wake ujuzi wa maisha kupitia masomo ya vitendo, hususan katika mchepuo wa kilimo.
Mwalimu Gideon John Mwakyoma, ambaye ni mmoja wa walimu wa somo la kilimo katika shule hiyo, ameendelea kuwalea na kuwaongoza wanafunzi kwa bidii katika bustani ya shule ambayo hutumika kama maabara ya wazi ya kujifunzia. Katika bustani hiyo, wanafunzi hujifunza hatua mbalimbali za uzalishaji wa mazao ya mboga mboga kuanzia maandalizi ya udongo, upandaji, umwagiliaji, ufuatiliaji wa ukuaji, hadi uvunaji.
“Tunataka wanafunzi wetu watoke hapa wakiwa na ujuzi wa kujitegemea, si tu kwa mitihani ya darasani bali pia kwa maisha halisi ya kila siku,” amesema Mwalimu Mwakyoma.
Bustani hizo zimekuwa sehemu muhimu ya kujifunzia ambapo mboga kama vile matembele, mchicha, na lettuce hulimwa na kutunzwa na wanafunzi wenyewe. Mbali na kujifunza kilimo, wanafunzi pia hujifunza nidhamu, kazi kwa bidii, na uwajibikaji kupitia shughuli hizo.
Wanafunzi waliohojiwa walieleza kufurahia somo hilo, wakisema kuwa linawasaidia kuelewa kilimo kama fursa ya ajira na chanzo cha kipato, hususan baada ya kuhitimu masomo.
Shule ya Sekondari Kibaha, chini ya Shirika la Elimu Kibaha, inaendelea kujikita katika utoaji wa elimu bora inayozingatia ujuzi, ubunifu na maadili, kwa lengo la kuwajenga vijana wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.