SERIKALI KUBORESHA UTOAJI WA ELIMU YA AFYA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA.

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Profesa Tumaini Nagu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kutekeleza uboreshaji wa miundombinu ya kutoa huduma katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI anayeshughulikia Afya, wakati alipotembelea Shirika la Elimu Kibaha kuona utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa madarasa, maabara na ofisi za wakufunzi wa chuo hicho.
“ Ofisi ya Rais-TAMISEMI inatambua kazi zinazotekelezwa na Shirika la Elimu Kibaha, na tupo pamoja katika kuboresha miundombinu ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha. Naomba Shirika liendelee kuwa kio katika mageuzi ya elimu kwa Taifa letu,” amesema Profesa Nagu.
Profesa Nagu amewataka viongozi na watumishi wa Shirika kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili mwanafunzi anayemaliza katika chuo hicho ajione tofauti na wanafunzi wengine kutokana na ujuzi na maarifa makubwa atakayokuwa amejifunza.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Tusekile Solile aliomba Serikali kuendelea kuboresha miundombinu ya utoaji wa huduma za afya katika chuo hicho ili Watanzania wengi wapate fursa ya kusoma elimu ya afya.
Pia, Profesa Nagu, alipokea taarifa fupi kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika, Bw. Anathe Nnko ya uanzishwaji wa KEC na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha, Profesa Nagu alitembelea madarasa pacha mawili yaliojengwa kwa fedha za mapato ya ndani na ujenzi wa jengo jipya la maabara ya kompyuta ambalo litagharimu zaidi ya shilingi milioni 80 ikiwa ni fedha zinazotokana na mapato ya ndani ya Shirika la Elimu Kibaha.
Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha, kinatoa kozi za Stashahada ya utabibu, Stashahada ya uuguzi na ukunga na Astashahada ya wahudumu wa Afya ngazi ya jamii.