Habari

Mahafali ya 55 yafanyika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha


Mahafali ya 55 ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha (KCOHAS) yamefanyika leo Ijumaa Agosti 05, 2022 katika viwanja vya chuo hicho na jumla ya wanafunzi 102 wakiwemo wanaume 44 na wanawake 55 wametunukiwa Stashahada ya fani ya uuguzi na ukunga.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wa chuo hicho, Bi. Gladness Salamba amemshukuru Mungu kwa wao kumaliza chuo salama na kueleza mafanikio, changamoto na mapendekezo ya yao kwa maendeleo ya chuo hicho.

“Chuo chetu ni miongoni mwa vyuo bora vya afya hapa nchini. Tulianza masomo yetu mwaka 2019 na leo hii baada ya miaka mitatu tunahitimu masomo yetu ya fani ya uuguzi na ukunga. Tumeweza kujifunza fani ya uuguzi na ukunga kwa nadharia na vitendo; kutoa elimu ya afya kwa jamii inayotuzunguka na vituo vya afya tulivyofanyia mazoezi kwa vitendo nje ya chuo hivyo kuongeza kiwango cha ufaulu kwa mitihani yetu ya ndani na nje ya chuo ambapo kwa mwaka 2019 chuo chetu kilikuwa cha kwanza kitaaluma kitaifa kwa vyuo vya Afya vya Serikali.” Alisema Bi. Gladness.

“Pamoja na mafanikio tuliyopata, pia tumekumbana na changamoto ya uchakavu wa miundombinu ya majengo ya chuo; wanafunzi kujitegemea katika gharama za chakula ambapo wakati mwingine ugumu wa maisha unasababisha baadhi yetu kutomudu masomo, upungufu wa vyumba vya madarasa, vya kulala na matundu ya vyoo ukilinganisha na idadi ya wanafunzi waliopo chuoni hapo.” Alisema Bi. Gladness.

Wakati huohuo, wahitimu hao walipendekeza wanafunzi wa vyuo vya afya vya kati wapewe mikopo na Serikali kama ilivyokuwa kwa vyuo vingine vya elimu ya juu; miundombinu ya majengo ya chuo iwe inakarabatiwa mara kwa mara na majengo ya vyumba vya madarasa, vyoo na mabweni iongezwe ili kuendana na idadi ya wanafunzi waliopo.

Akizungumza katika mahafali hayo, mgeni rasmi ambaye ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Dkt. Charles Msonde amewapongeza wahitimu hao na kuwataka kuzingatia maadili wanapokwenda kufanya kazi za kuimarisha afya za watanzania. Pia ametoa wito kwa wahitimu hao kujiendeleza zaidi katika fani yao.

“Kada za afya ni tofauti na kada nyingine yoyote katika taifa lolote duniani kwa sababu kada hizi za afya zinaenda kuhudumia afya na maisha ya mtu, ukifanya kosa kidogo kwenye kazi hii unaharibu maisha ya mtu moja kwa moja.” Alisema Dkt. Msonde.

“Ndiyo maana Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inafanya jitihada kubwa za kuimarisha maeneo mbalimbali ya afya kwa kutoa fedha kwa ajili ya kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali nchini, lengo ni kuhakikisha kwamba huduma ya afya inatolewa vizuri, kwenye mazingira mazuri na kwa umakini mkubwa.” Alisema Dkt. Msonde.

Dkt. Msonde pia alitumia nafasi hiyo kuwaalika wadau mbalimbali kuwekeza katika ujenzi wa Chuo cha KCOHAS, ili kujenga majengo ya kisasa kwa miundombinu bora ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi na wakufunzi wa chuo hicho, kwani Shirika la Elimu Kibaha limetenga eneo lenye ukubwa wa ekari 100 kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho kwa kujenga majengo mapya.

Mahafali hayo ya 55 ya Chuo cha KCOHAS yamehudhuriwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Bi. Chiku Wahady, Mganga mfawidhi wa Hospitali teule ya Mkoa wa Pwani Tumbi, Mkuu wa Chuo cha KCOHAS. Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Shirika la Elimu Kibaha, wakufunzi na watumishi wasio wakufunzi wa KCOHAS, viongozi wa dini, wanafunzi na wazazi wa wahitimu wa chuo hicho.