Maktaba ya Umma Kibaha
Maktaba ya Umma Kibaha (KPL) ni kitengo kimojawapo ambacho kinawajibika kwenye Kurugenzi ya Huduma za Elimu ndani ya Shirika la Elimu Kibaha. Kwa kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa Shirika la Elimu Kibaha (SEK) ni kuwa kituo cha mfano nchini Tanzania katika kupambana na ujinga, maradhi na umaskini, ifuatayo ni: dira ya KPL; dhima ya KPL; kanuni ya msingi ya KPL; wito wetu kwa watumiaji wa KPL; kanuni na taratibu za msingi za KPL; pamoja na huduma za msingi ambazo zinatolewa kwa sasa na KPL; na huduma zinazotarajiwa kutolewa hapo baadaye.
DIRA YA KPL
Kiu kuu ya KPL ni kuwa kituo cha kisasa cha utoaji huduma za maktaba na cha kuelimisha, kuwasiliana na kuburudisha umma wa SEK, Mji wa Kibaha na viunga vyake pamoja mkoa mzima wa Pwani na mikoa jirani kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii, kiutamaduni, kiuchumi, kitaaluma na kimaendeleo kwa kushirikiana na Maktaba ya Umma ya Mkoa Pwani.
DHIMA YA KPL
Jukumu kuu la KPL ni kutumia huduma mbalimbali zinazotolewa kuwawezesha watumiaji wa huduma husika kupiga vita wao wenyewe: ujinga; maradhi; umaskini na uasi wa kila namna kwa manufaa yao wenyewe kwanza kisha kwa manufaa ya jamii na taifa letu kwa ujumla.
KANUNI YA MSINGI YA KPL
KPL inamjali sana kila mteja, kwa maana ya kila mtumiaji wa huduma zinazotolewa na maktaba, kwa sababu tunaamini kwamba ni mteja tunayemhudumia ndiye anahalalisha KPL kama kitengo kuwepo.
WITO WA KPL KWA WATUMIAJI WA HUDUMA ZETU
Ndugu mtumiaji wa huduma za KPL, karibu sana ili utupatie fursa ya kukuonyesha namna gani unaweza kupiga vita wewe mwenyewe: ujinga; maradhi; umaskini na uasi wa kila namna kwa kutumia huduma zinazotolewa kadri unavyoweza kwa kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa
HUDUMA AMBAZO KPL INATARAJIA KUANZA KUTOA KARIBUNI
Utoaji wa huduma ya intaneti pamoja na fotokopi kwa gharama nafuu.
Huduma za video na redio kwa ajili ya watoto wadogo.
Utoaji wa huduma za maktaba kwa njia za kielektroniki.
Maonyesho ya huduma zetu kwenye hafla mbalimbali za kimkoa kwenye Mkoa wa Pwani