Shirika la Elimu Kibaha latoa mafunzo ya e-Mrejesho kwa viongozi

Shirika la Elimu Kibaha, limetoa mafunzo ya e-Mrejesho kwa viongozi wa Shirika kwa lengo la kuwawezesha kutumia mfumo huo, kupokea na kujibu kwa wakati taarifa za malalamiko, mapendekezo, maulizo, ushauri na pongezi kutoka kwa wananchi.
Katika mafunzo hayo, viongozi walijifunza jinsi ya kushughulikia mrejesho kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa na Shirika pamoja na kujifunza kuingia kwenye mfumo wa e-Mrejesho.
Akitoa mada kuhusu utumiaji wa e-Mrejesho, Afisa TEHAMA, Bw. Amran Ramadhan alisema kila mtumiaji anapaswa kuingia kwenye mfumo wa e-Mrejesho na kushughulikia mrejesho uliotumwa na wananchi kuhusiana na huduma zinazotolewa na Shirika la Elimu Kibaha.
“Mfumo huu, unawarahisishia wananchi kutuma mrejesho wa huduma zinazotolewa na Shirika na kupata majibu kwa haraka na kwa ufanisi zaidi,” alisema Bw. Ramadhan.
Akitoa mada kuhusu Mkataba wa Huduma kwa Mteja ambao ni msingi wa utoaji huduma kwa wananchi, Bw. Emmanuel Lweyo alisema mkataba huo unainisha muda wa kushughulikia huduma ambazo mwananchi anazitaka kutoka katika taasisi zilizopo chini ya Shirika.
Bw. Lweyo alisisitiza kwamba watumishi wa Shirika wanatakiwa kuzingatia viwango vya huduma vilivyoanishwa katika mkataba huo ili kutoa huduma bora zaidi kwa umma.
Mfumo wa e-Mrejesho utawawezesha viongozi na maofisa wengine wa Shirika kutumia mfumo huo na kuona kwa wakati ushauri, malalamiko na pongezi zinazotumwa na wananchi.
Shirika la Elimu Kibaha linatoa huduma za elimu, mafunzo na huduma za maktaba kwa umma kupitia taasisi zake ambazo ni shule na vyuo vya kati.