Habari
Shirika la Elimu Kibaha lapongezwa kwa utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo.
Kamati ya Bodi ya Wakurugenzi ya Uwekezaji, bajeti na maendeleo ya Shirika la Elimu Kibaha ikiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Bi. Theresia Henjewele jana siku ya Alhamisi tarehe 21/10/2021 imefanya ziara ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo minne (4) iliyopo katika Shirika la Elimu Kibaha.
Katika ziara hiyo, Bi. Henjewele ameipongeza menejimenti ya Shirika la Elimu Kibaha kwa maendeleo mazuri ya utekelezaji miradi hiyo na kuwataka kusimamia kwa karibu zaidi ili miradi hiyo ikamilike ndani ya muda uliopangwa.
Kamati hiyo iliweza kutembelea mradi wa Ujenzi wa mabweni matatu (3) katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Kibaha wenye gharama ya shilingi milioni mia mbili na arobaini (Tsh. 240,000,000)unaotekelezwa kwa fedha kutoka Serikali kuu chini ya Mpango wa EP4R na mradi wa ukarabati wa majengo ya shule na ujenzi wa vyumba vitatu (3) vya madarasa Shule ya Msingi Tumbi wenye gharama ya shilingi milioni mia mbili themanini na moja, laki nane na elfu tano mia nane na ishirini na tisa (Tsh. 281,805,829)unaotekelezwa kwa fedha kutoka Serikali kuu chini ya Mpango wa EP4R.
Pia kamati ilitembelea na kukagua ujenzi wa jengo la madarasa la ghorofa moja shule ya sekondari Kihaha lenye bajeti ya shilingi milioni mia sita (Tsh. 600,000,000) unaotekelezwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Shirika la Elimu Kibaha na michango mbalimbali ya wadau ambapo mpaka sasa jumla ya shilingi milioni thelathini na sita (Tsh. 36,000,000) zimeshatolewa na kutumika.
Ziara hiyo pia ilihusisha ukaguzi wa mradi wa mabwawa ya majitaka ambayo Shirika la Elimu Kibaha imeubuni na kuwa moja ya chanzo cha mapato ya ndani ya Shirika. Mradi una bajeti ya shilingi milioni nne, laki tisa na elfu mbili na mia nane (Tsh. 4,902,800) ambapo fedha hiyo inatokana na mapato ya ndani ya Shirika na itahusisha kukarabati na kusafisha mabwawa matatu ya maji taka, ujenzi wa geti na chumba cha mlinzi ambapo shirika litakuwa likitoa huduma hiyo kwa mkoa wote wa Pwani.