Habari
Shirika la Elimu Kibaha latoa msaada kwa wahanga wa moto Mkuza
Shirika la elimu Kibaha kupitia wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha leo Jumatano tarehe 25/05/2022 wametoa msaada wa vifaa vya kujisomea kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkuza iliyopatwa na janga la kuunguliwa moto moja ya bweni la wanafunzi wake tarehe 15/05/2022.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha Bw. Jonas Mtangi amewapa pole uongozi wa shule, walimu pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkuza kwa janga la moto lililowapata.
Poleni sana kwa kuunguliwa bweni la wanafunzi, tunajua wanafunzi walikuwa wamehifadhi vitu ikiwa ni pamoja na vifaa vya kusomea, leo kupitia Shule yetu ya Sekondari Kibaha, tumeleta msaada wa vitabu vya masomo mbalimbali na baadhi ya mitihani ya kurejea ili wanafunzi wahanga wa moto waweze kupata urahisi wa kujisomea.” Alisema Bw. Mtangi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mkuza Bi. Mercy Nkya ameeleza kuwa chanzo cha moto mpaka leo hakijajulikana, na moto huo umeteketeza vitu vyote vilivyokuwemo kwenye bweni hilo kwa siku hiyo.
“Moto huo ulitokea siku ya Jumapili tarehe 15 mwezi huu wa tano majira ya jioni wanafunzi wakiwa wanasali, vitu vyote vilivyokuwemo kwenye bweni hili vimeteketea na moto huo na hakuna mwanafunzi yeyote aliyejeruhiwa katika moto huo kwa kuwa hawa kuwepo bwenini.” Alisema Bi. Nkya.
Akikabidhi msaada huo, Kaka Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha, Abdulkadirn Massa amesema kuwa, vifaa hivyo wanavikabidhi kwa wanafunzi wahanga wa moto wa Shule ya Sekondari Mkuza ili viwasaidie kitaaluma.
Naye, Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Mkuza, Elista Thomas ameshukuru kwa msaada huo na kuahidi kutumia vyema vifaa vyote walivyopewa.