Habari

Wafanyakazi Bora Shirika la Elimu Kibaha wapatiwa zawadi


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Bw. Anathe Nnko tarehe 01/05/2023 amekabidhi zawadi kwa watumishi sita wa Shirika hilo waliochaguliwa kuwa wafanyakazi bora kwa mwaka 2023.

Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi hizo, Bw. Nnko amewapongeza watumishi hao na kuwataka kuongeza bidii zaidi na zawadi hizo ziwaongezee morali ya utendaji wao wa kazi.

“Namshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuifikia siku hii ya leo. Historia ya maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani imesaidia sana kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi.”

“Wafanyakazi wote wa Shirika la Elimu Kibaha ni watendaji kazi wazuri, lakini ninyi mmeonekana hodari zaidi kwa mwaka huu, hivyo tunawapongeza na zawadi hii iwaongezee morali ya kufanya kazi zaidi, hongereni sana” amesema Bw. Nnko.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi waliopata zawadi hizo, Bw. Rashidi Mswahili ametoa shukurani kwa watumishi na uongozi wote wa Shirika la Elimu Kibaha kwa kutambua juhudi zao na kuwachagua kuwa wafanyakazi bora.

“Nawashukuru wafanyakazi na uongozi wa Shirika la Elimu Kibaha kwa kututambua na kutuchagua kuwa wafanyakazi bora. Dunia inaenda haraka na inabadilika sana, hivyo sisi wafanyakazi pia tunatakiwa kubadilika na kuwa wabunifu, wenye nidhamu na ushirikiano baina yetu ili tufikie malengo yetu na ya taasisi kwa ujumla”, amesema Bw. Richard Mswahili.

Watumishi waliopatiwa zawadi kwa kutambuliwa kuwa wafanyakazi bora ni Bw. Richard Mswahili, Dkt. Janeth Cassian, Mhandisi Godfrey Kisonga, Bw. Afraha Hassan, Bi. Cresencia Shirima na Bw. Robert Kanyawawa.

Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani kwa mwaka huu 2023, kwa Mkoa wa Pwani yamefanyika katika Wilaya ya Chalinze, kauli mbiu ikiwa “Mishahara bora na ajira za staha ni nguzo kwa maendeleo ya wafanyakazi. Wakati ni sasa”.