Historia

Shirika la Elimu Kibaha ni Shirika la umma linalotoa huduma mbalimbali, lipo Mkoa wa Pwani kilomita 40 magharibi mwa Mji wa Dar es salaam, pembezoni mwa barabara Kuu iendayo Morogoro. Shirika la Elimu Kibaha lilianzishwa mwaka 1963 kama mradi wa pamoja chini ya wafadhili watano- Serikali ya Tanganyika kwa kipindi hicho kwa upande mmoja pamoja na nchi nne za Kinordic (Dernmark, Norway, Finland na Sweden) kwa upande mwengine. Kwa kipindi hicho mradi huu ulijulikana kama “Tanganyika Nordic Project” mpaka mwaka 1970 ambapo mradi huu ulikabidhiwa rasmi kwa Serikali ya Tanzania na kuitwa Shirika la Elimu Kibaha. Na kusajiwa chini ya sheria ya Mashirika ya Umma Na.17 ya mwaka 1969, marejeo ya mwaka 2002.

Shirika la Elimu Kibaha linaongozwa na Bodi ya Wakurugenzi, ambayo mwenyekiti wake huteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkurugenzi Mkuu wa Shirika ambaye ndiye mtendaji mkuu na Katibu wa Bodi hiyo, huteuliwa na Waziri mwenye dhamana husika ya kulisimamia Shirika ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI). Wajumbe Wabodi ya Shirika huteuliwa kutoka katika Wizara ya Kilimo na Ufugaji, Wizara ya Afya, Jinsia na Maendeleo ya Jamii, Wizara ya Elimu na Ufundi Stadi, Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na mwakilishi kutoka OR-TAMISEMI na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha.