MAHAFALI YA 24: Mgeni rasmi ahaidi neema Shule ya Sekondari Tumbi.

Mgeni rasmi, Bw. Saidi Machinga, ametoa hundi ya shilingi milioni 10 kwa ajili ya ukarabati wa jengo la utawala la Shule ya Sekondari Tumbi wakati wa mahafali ya 24 ya wahitimu wa kidato cha nne wa Shule hiyo.
Mahafali hayo yamefanyika leo tarehe 26. 09.2025 kwenye Viwanja vya Shule ya Sekondari Tumbi na kuudhuriwa na wageni mbalimbali.
Kiasi hiki kinatarajiwa kusaidia kwa asilimia kubwa katika kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, sambamba na kutatua changamoto zinazokabili shule hiyo,” alisema Bw. Machinga.
Mbali na kutoa fedha hizo, Bw. Machinga ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Usafirishaji ya Sakalista, ameahidi kujenga jengo la maktaba katika shule hiyo.
Aidha, Bw. Machinga ameahidi kutoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi watakaofanya vyema katika mitihani yao ya mwisho, hatua ambayo inalenga kuwahamasisha wanafunzi kuongeza bidii katika masomo yao.
Katika mahafali hayo, Bw. Boss Kwezi aliwataka wanafunzi wanaohitimu kuwa na nidhamu, kuwaheshimu walimu pamoja na kusikiliza ushauri wa wazazi ili kufikia mafanikio katika maisha yao ya baadaye.
Alisisitiza kuwa misingi bora waliyojengewa na walimu wa shule hiyo itawasaidia endapo wataendelea kuithamini na kuizingatia.
Naye, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Elimu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Jonas Mtangi alitoa pongezi kwa walimu, wazazi na uongozi wa shule kwa ushirikiano wao ambao umechangia mafanikio chanya katika taaluma ya shule hiyo.
Vilevile, alimshukuru Bw. Saidi Machinga kwa kukubali kuwa mgeni rasmi na kusaidia maendeleo ya shule hiyo.
Mahafali hayo yameacha alama kubwa kwa shule ya Tumbi, yakiwa ni kielelezo cha mshikamano kati ya shule, jamii, na wadau mbalimbali wa elimu.