Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Shirika La Elimu Kibaha

SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA LAPOKEA MSAADA WA MAABARA YA KOMPYUTA NA SOLAR PANEL.

Imewekwa: 16 Oct, 2025
SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA LAPOKEA MSAADA WA MAABARA YA KOMPYUTA NA SOLAR PANEL.

Kibaha, 16 Oktoba 2025 – Shule ya Sekondari Kibaha, inayosimamiwa na Shirika la Elimu Kibaha (KEC), imepokea msaada wa maabara ya kompyuta 31 na paneli za sola 30 zenye thamani ya Shilingi milioni 166.97, kutoka kwa wanafunzi waliowahi kuhitimu katika shule hiyo kwa kushirikiana na Bw. Abdul Mombokaleo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya makabidhiano ya vifaa hivyo.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Bw. Mombokaleo alisema msaada huo unalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi pamoja na kuchochea matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu nchini.

"Ni matumaini yetu, vifaa hivi vitawawezesha wanafunzi kujifunza kwa ufanisi zaidi na kuwa na ujuzi wa kisasa utakaowasaidia katika maisha yao ya baadaye," alisema Bw. Mombokaleo.

Aidha, aliwashukuru viongozi wa shule hiyo kwa kumchagua kuwa mgeni rasmi kwa awamu ya pili mfululizo, na akaahidi kuendelea kuisaidia shule hiyo kwa hali na mali. 

Bw. Mombokaleo aliwataka wanafunzi kuvitumia vifaa hivyo kwa manufaa yao, kuvilinda, na kuendeleza moyo wa kuwasaidia wengine kama njia ya kurejesha fadhila kwa taasisi iliyowawezesha kufika hapo walipo.

Katika hotuba yake kwa wanafunzi, aliwaasa kuzingatia mambo matano muhimu ya kimaadili katika maisha yao ya kila siku.

Bw. Mombokaleo alitaja mambo matano kuwa ni; kuipenda nchi yao ya Tanzania, kuwa wakarimu, kuwa jasiri, kuwa wapatanishi, na kuwa na moyo wa shukrani.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Elimu wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Jonas Mtangi alieleza kufurahishwa na mchango mkubwa wa vifaa vya TEHAMA  na kwamba vitachangia katika kuboresha ujifunzaji wa wanafunzi wa shule hiyo.

Pia, alitumia nafasi hiyo kuwapongeza walimu na wazazi kwa mshikamano wao katika kuhakikisha maendeleo ya wanafunzi wa shule hiyo yanaendelea kuwa mazuri.

Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Robert Shilingi, alimpongeza Bw. Mombokaleo kwa juhudi zake za kuwaunganisha wahitimu walisoma katika shule hiyo na kufanikiwa kutoa msaada wa kompyuta na kukarabati chumba cha maabara ya kompyuta .

Bw. Shilingi alisema kwa kushirikiana na mamlaka atawapatia eneo maalum kwa ajili ya kuendesha shughuli zao za kiofisi ndani ya Idara ya Maendeleo ya Jamii.

Bw. Shilingi alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi wote kushiriki Uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu, akisisitiza kuwa hali ya usalama nchini ni shwari na kuruhusu wananchi kutimiza haki yao ya kikatiba kwa uhuru.

Kwa pamoja, uongozi wa Shule ya Sekondari Kibaha na Menejimenti ya Shirika la Elimu Kibaha walitoa shukrani za dhati kwa wahitimu waliowahi kusoma katika shule hiyo kwa msaada huo na aliahidi kwamba vifaa hivyo vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuboresha elimu na maisha ya wanafunzi.