MABALOZI WA SWEDEN, NORWAY, DENMARK NA FINLAND WATEMBELEA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA.

Mabalozi wanne kutoka nchi za kinodiki, Sweden, Norway, Denmark na Finland wamefurahishwa na hatua kubwa ya maendeleo yaliyofanywa na Serikali ya Tanzania baada ya nchi hizo kungana mwaka 1963 na kuanzisha mradi wa kupambana na maadui watatu wa maendeleo; Ujinga, Umaskini na Maradhi.
Kauli hiyo imetolewa leo tarehe 10/10/2025 wakati mabalozi hao walipotembelea Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kuona miradi ya elimu iliyoanzishwa na nchi hizo kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania.
Balozi wa Finland nchini Tanzania, Bi. Theresa Zitting alisema Shirika la Elimu Kibaha limefanikiwa kuongeza miundombinu ya utoaji wa elimu ukilinganisha na mwaka 1963 wakati KEC ilipoanzishwa.
”Nimefurahi kulitembelea Shirika la Elimu Kibaha, naona kuna maendeleo makubwa, KEC imekuwa kubwa,” alifafanua Bi. Theresa.
Balozi wa Sweden nchini Tanzania, Bi. Charlotta Ozaki Macias alisema Serikali ya Sweden itaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika uboreshaji wa elimu ya msingi, sekondari na vyuo.
”Tangu miaka 1960, tumekuwa tukishirikiana na Tanzania katika utoaji wa huduma za elimu,” alisema Bi. Charlotta.
Naye, Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Bw. Jesper ... alibainisha kuwa KEC imekuwa mfano katika utoaji wa elimu bora nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Robert Shilingi alifurahishwa na ujio wa wageni hao na kubainisha kwamba KEC itaendelea kushirikiana na nchi hizo katika kuendeleza miradi ya huduma za elimu katika shirika hilo.
”Ugeni huu, umetutia moyo wa kuendelea kufanya kazi kwa bidii na tutaendelea kubuni miradi mbalimbali ya elimu kwa sababu tuna fursa za kutosha,” alisema Bw. Shilingi.
Awali baada ya kuwakaribisha mabalozi hao, Bw. Shilingi alitoa historia fupi ya Shirika la Elimu Kibaha tangu kuanzishwa kwake hadi kufikia mafanikio ya sasa.
Bw. Shilingi alisema miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuanzishwa kwa shule mbili za kutwa ambazo ni Shule ya Sekondari Tumbi na Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha, ambazo zimeendelea kutoa mchango mkubwa katika kuinua kiwango cha elimu mkoani Pwani na nchini kwa ujumla.
Aidha, alisema mchango mkubwa wa Nordic Teacher Association – Kibaha (KNTA), umekuwa chachu ya kuleta maendeleo na mapinduzi makubwa katika sekta ya elimu, kwa kutoa fursa mbalimbali za mafunzo na kubadilishana uzoefu baina ya walimu wa Tanzania na wa nchi za kinodiki.
Katika hotuba yake ya kufunga, Bw. Shilingi alitoa shukrani za dhati kwa wageni hao kwa kutembelea shirika hilo.
“Tutafanya kila jitihada za kuitumia ipasavyo fursa hii ambayo imeletwa na juhudi za pamoja kati yetu na nchi za kinodiki, Pia, tutajitahidi kwa uwezo wetu wote kuhakikisha sehemu hii inabaki kuwa kumbukumbu hai na ya heshima ya ushirikiano wa kimataifa alisema Bw. Shilingi.
Bw. Shilingi aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia na nchi za kinodiki.
"KEC inapenda kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa juhudi zake za kudumisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi za kinodiki pamoja na dunia kwa ujumla. Ni kupitia juhudi hizi, ushirikiano kama huu unaendelea kuimarika na kuleta manufaa makubwa kwa Taifa letu," alisema Bw. Shilingi.