‘VIJANA WA KIBAHA-FDC WAMEIVA, TUMIENI UJUZI WENU KUJIAJIRI’
Wahitimu 112 wa kozi mbalimbali za ujuzi na ufundi stadi leo tarehe 20/11/2025 wamekabidhiwa vyeti katika mahafali ya 53 ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha yaliofanyika kwenye Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.
Mgeni rasmi katika mahafali hayo, Mkurugenzi wa Kampuni ya Ngure, Bw. Elisante Joakim Ngure aliahidi kufanyia kazi changamoto zilizowasilishwa na wahitimu kupitia risala yao.
“Changamoto hizi nitazifikisha kwenye mamlaka husika ili kupata ufumbuzi wenye tija kwa chuo chetu na kwa vijana wanaosoma hapa,” alisema Bw. Ngure.
Kabla ya kutoa hotuba yake, mgeni rasmi alitembelea maonesho ya kazi za vitendo yaliyoandaliwa na wanafunzi wa Kibaha-FDC.
Katika maonesho hayo, Bw. Ngure alionesha kufurahishwa na ubunifu na umahiri kupitia maonesho ya ushonaji na ubunifu wa mavazi, ufundi umeme na ufundi bomba.
“Maonesho haya ni ishara tosha vijana wameiva katika fani walizofundishwa, na hivyo wako tayari kwenda kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za uzalishaji,” alisema Bw. Ngure.
Bw. Ngure aliwashauri wahitimu kutumia ujuzi waliopata chuoni hapo kama njia ya kupunguza changamoto ya ajira, akiwataka kujitambua na kuwa wabunifu katika kuanzisha miradi ya kujiajiri.
Pia, aliwapongeza walimu wa Kibaha- FDC kwa juhudi kubwa wanazoweka ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu na mafunzo bora.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Bw. Damas Msaki, aliwakumbusha wahitimu kuonesha kile walichojifunza.
“Muda wa kujitegemea umefika—nendeni mkatoe huduma bora huko muendako,” alisema Bw. Msaki.
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Elimu, Bw. Jonas Mtangi, aliupongeza uongozi wa chuo, walimu, pamoja na wazazi kwa kushirikiana katika utoaji wa mafunzo ya ujuzi na ufundi stadi ambao umewawezesha wahitimu kuwa wabunifu katika fani mbalimbali wailizosoma.
Mahafali hayo yamehudhuriwa na wazazi, walezi, wadau wa elimu na wanafunzi.