Habari

​28 Wahitimu Udereva Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha


Wanafunzi 28 wa kozi fupi ya udereva leo tarehe 03/06/2022 wamefanya sherehe ya kuhitimu mafunzo hayo yaliyofanyika katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC).

Mgeni rasmi katika mahafali hayo ambaye ni Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha Bw. Joseph Nchimbi, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii katika Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Anathe Nnko, amewapongeza wahitimu hao kwa kuamua kwenda chuoni hapo kupata elimu ya udereva na amewataka kuonyesha weledi walionao kwa kujitofautisha na wengine ambao hawajapata mafunzo rasmi.

“Unapohitimu fani hii ya udereva na kuifanyia kazi, unatoa mchango mkubwa kwa uchumi wa jamii na nchi kwa ujumla kwa kusafirisha watu au mizigo, kusaidia kuokoa muda na kutoa huduma kwa wakati. Pia ni fani inayotupatia vipato kwa kujiajiri au kuajiriwa.”

“Kozi ya udereva ni moja ya kozi zinazotolewa na KFDC, chuo hiki kina wajibu wa kutoa ufahamu na kuongeza ujuzi kwa wananchi, na moja ya ujuzi tunaotoa ni fani ya udereva. Mfuate na mheshimu alama za barabarani kwa kuwa zinatuongoza na kutupa tahadhari mbalimbali ili kukuokoa wewe na watu waliopo eneo unalopita.” Amesema Bw. Nchimbi.

Pia Bw. Nchimbi, ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha tena wahitimu hao katika chuo hicho kwa kuwa chuo hicho kinatoa elimu ya fani nyingine zaidi ya udereva zikiwemo ushonaji na ubunifu wa mavazi, uwashi, ufundi wa umeme majumbani, upishi na usimamizi wa hotelia, ufundi wa magari, ufundi bomba, kilimo, mifugo, ufundi wa uundaji na uungaji wa vyuma, useremala, kilimo cha bustani na ufugaji wa kuku.

Akizungumza kwa niaba ya wahitimu wenzake, Bw.Brayson Gadau, ameushukuru uongozi wa chuo na wakufunzi wa fani ya udereva kwa ushirikiano waliowapa tangu wameanza kozi hiyo fupi ya miezi miwili mpaka wanahitimu.

“Tunashukuru kwa ushirikiano na ujuzi tulioupata hapa chuoni, na tunaahidi tutakuwa madereva hodari ambao tutazingatia vema mafunzo yote tuliyopewa.” Amesema Bw. Gadau.

Sherehe hiyo imeambatana na utoaji wa vyeti kwa wahitimu pia imehudhuriwa na makamu mkuu wa Chuo cha KFDC, Bi. Cresencia Shirima; Mkufunzi Mkuu wa fani ya udereva Hamisi Razaro, wakufunzi wa Chuo cha KFDC na wanafunzi wa chuo hicho.