Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Shirika La Elimu Kibaha

MAHAFALI YA 54, SHULE YA MSINGI TUMBI YAAHIDIWA KOMPYUTA 20.

Imewekwa: 01 Oct, 2025
MAHAFALI YA 54, SHULE YA MSINGI TUMBI YAAHIDIWA KOMPYUTA 20.

 Shule ya Msingi Tumbi imepata neema katika Mahahfali ya 54 baada ya Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania, Bw. Abdul Mombokaleo

 kuahidi kutoa msaada wa kompyuta 20, skrini janja (smart board), pamoja na kutoa bure  huduma ya intaneti  kwa mwaka mzima kwa ajili ya shule hiyo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Mombokaleo — ambaye amesoma katika shule hiyo— alisema msaada huo ni sehemu ya mchango wake katika kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa Shuke ya Msingi Tumbi.

Alisema matumizi ya  teknolojia katika elimu ya sasa ni muhimu  na kuwekaza katika elimu ni msingi wa maendeleo ya Taifa.

Katika hotuba yake, aliwashukuru walimu na wazazi kwa ushirikiano wao katika kulea na kuelimisha watoto.

Alisema kuwa kurejea katika shule aliyosoma kama mgeni rasmi ni heshima kubwa kwake, na ni ishara ya mshikamano wa kijamii unaopaswa kuenziwa.

Aliwahimiza wanafunzi kuwa wajasiri, wasikate tamaa, wawe na nidhamu, ukarimu  na kuwashukuru wazazi na walezi wanaowalea.

Mkuu wa shule hiyo, kwa upande wake, alitoa shukrani kwa wazazi kwa mchango wao mkubwa katika safari ya kielimu ya wanafunzi, hadi kufikia hatua ya kuhitimu darasa la Saba.

Bw. Jani alimshukuru mgeni rasmi,  Bw. Mombokaleo kwa kukubali mwaliko huo na zawadi aliyopewa.

Kaimu Mkurugenzi wa kurugenzi ya elimu Elimu, Bw. Jonas Mtangi alihitimisha kwa kuwasisitiza wazazi kuendelea kushirikiana na walimu, huku akiwahimiza wanafunzi kuthamini na kutumia kwa vitendo mafunzo waliyoyapata shuleni, hata wakiwa nje ya shule hiyo.

Mahafali hayo yalihudhuriwa na wazazi, walimu, viongozi wa elimu, pamoja na wageni mbalimbali, na yalionyesha wazi mafanikio ya mshikamano kati ya jamii na shule katika kuimarisha elimu bora kwa watoto.