ASASI YA KIRAIA YA UHOLANZI INAYOITWA GERED GEREEDSCHAP YAIPATIA SHIRILKA LA ELIMU KIBAHA VIFAA VYA KUFUNDISHIA.
Asasi ya Kiraia ya Uholanzi, GERED GEREEDSCHAP yaipatia Shirika la Elimu Kibaha vifaa vya kufundishia
Asasi isiyo ya Kiserikali ya Uholanzi imeonesha dhamira yake ya kuunga mkono maendeleo ya elimu nchini Tanzania kwa kuipatia Shirika la Elimu Kibaha (KEC), vifaa na mashine mbalimbali za kisasa ili kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia, kwa Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi (KFDC).
Msaada huo umetolewa na asasi hiyo ya GERED GEREEDSCHAP kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya vitendo sambamba na nadharia kwa wanachuo wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha.
Lengo utoaji wa msaada huo ni kuwawezesha wanachuo kupata ujuzi unaoendana na mahitaji halisi ya soko la ajira nchini.
Vifaa hivyo pia vitasaidia walimu kufundisha kwa ufanisi zaidi, huku vikitoa fursa pana ya kuibua na kukuza vipaji miongoni mwa wanachuo wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Bw. Damas Msaki amewashukuru wafadhili hao na kueleza kuwa msaada huo ni chachu ya kuinua ubora wa elimu ya ufundi na maendeleo ya jamii.
"Msaada huu utaongeza uwezo wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha katika kuzalisha wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na ushindani," amesema Bw. Msaki.
Aidha, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha, Bw. Joseph Nchimbi amesema kuwa mashine hizo zitachochea utafiti mdogo na ubunifu wa kiteknolojia kwa vijana wanaosoma katika chuo hicho.
Hatua hii, inaakisi pia ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali ya Uholanzi na taasisi zake kwa kukuza elimu hapa nchini, ikiwa na lengo la kuwekeza katika rasilimali watu kama nguzo kuu ya maendeleo endelevu ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Msaada huo wa mashine na vifaa mbalimbali vya Ufundi pamoja na kasha (container) vimepokelewa Jana tarehe 26/02/2026 katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KIBAHA-FDC) ambacho kipo chini ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC)