Habari

​Changamoto za walimu watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha zapatiwa ufumbuzi


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora Dkt. Francis Michael, leo tarehe 20/08/2021 amefanya kikao cha kusikiliza na kuzipatia majibu na ufumbuzi changamoto zinazowakabili walimu watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha.

Akisoma risala ya walimu hao kwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora, Bi. Mwajuma Peresi, kwa niaba ya Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Pwani, ameeleza changamoto walizonazo walimu watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha na kuomba Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora kusaidia katika mapitio ya sheria na kanuni za uundwaji wa bodi ya kitaalamu ya Walimu ambazo hazionyeshi tija.
"Changamoto hizo ni pamoja na ulipwaji wa malimbikizo ya mishahara, ulipwaji wa madeni mbalimbali yaliyokwisha kuhakikiwa na yale ambayo hayajahakikiwa; miundo ya kiutumishi na malipo ya fedha za likizo yasiyokidhi haja. Amesema Bi. Peresi.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora Dkt. Francis Michael, amewaeleza walimu wa Shirika la Elimu Kibaha kuwa, katika dhana ya kusikiliza na kutatua changamoto za watumishi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI wamekuja na njia mbalimbali za kusikiliza changamoto hizo kwa kuanzisha namba maalum ambazo watumishi watazitumia kupiga simu na kueleza changamoto zao na kupatiwa utekelezaji wake.
"Tuna namba ambazo mtumishi ukipata shida za kiutumishi unaruhusiwa kupiga na ukapata ufafanuzi. Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora unapiga namba 0262160240 au 0734986508; Ofisi ya Rais TAMISEMI 0262160210." Amesema Dkt. Michael.
Pia Ofisi ya Rais Utumishi tuna Application ya SWUU ambayo unaweza kuiweka kwenye simu yako na kuwasiliana na Mhe. Waziri wa Utumishi na Utawala bora kwa kumtumia ujumbe au sauti."
Dkt. Michael pia ametoa ufafanuzi kuhusu muundo uliotokana na waraka wa msajili wa hazina wa mwaka 2010 ni kweli umesababisha kutokea kwa tofauti ya muundo wa mishahara ya watumishi walimu waliopo katika taasisi. Kutokana na changamoto hiyo, Serikali kupitia ofisi yangu imeamua kuja na muundo mmoja kwa watumishi wote walimu ambao utaondoa tofauti zilizopo.
Kuhusu malimbikizo ya mishahara

"Tumekubali kuna matatizo katika malipo ya malimbikizo ya mishahara, nakiri tatizo hilo kuwa lipo na linafanyiwa kazi na litatatuliwa kwa kiwa ndiyo matakwa ya Mhe. Rais wetu kuwa madeni ya mishahara kwa watumishi wote yalipwe." Amesema Dkt. Michael.
Katika kikao hicho, Dkt. Michael aliwaruhusu walimu kuzungumza changamoto nyingine walizonazo ili zitafutiwe ufumbuzi ambapo walimu walieleza changamoto walizonazo zikiwemo walimu wa ajira mpya kutopata mishahara yao kutokana na muundo mpya uliopo kwenye mfumo wa mishahara kutotambua vyeo vilivyopo na malipo ya likizo za walimu kutolipwa kwa wakati.
Kupitia changamoto hiyo, Dkt. Michael ameelekeza watumishi hao kuombewa kibali cha kupata mishahara binafsi mpaka pale muundo mpya utakapoanza kufanya kazi.
Kikao hicho kutatua changamoto za walimu kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shirika la Elimu Kibaha na kimeandaliwa na Chama cha Walimu Tanzania (CWT) ambapo kilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora, Mkurugenzi Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wakurugenzi wasaidizi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora sehemu za mishahara na utawala na Utumishi wa umma, kamati ya uongozi menejimenti ya Shirika la Elimu Kibaha na Walimu watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha.