Habari

Dkt. Jafo akabidhi milioni 50 kwa walimu Tumbi Sekondari


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Selemani Jafo leo amekabidhi Shilingi milioni 50 kwa walimu wa Shule ya Sekondari Tumbi inayomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kwa kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa shule hiyo na kuipongeza kuwa shule ya kata ya kwanza nchini kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne mwaka 2022.

Dkt. Jafo amekabidhi fedha hizo kwa walimu wa Shule ya Sekondari Tumbi ikiwa ni kutimiza ahadi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango aliyoitoa tarehe 04/02/2023 wakati walipofika katika shule hiyo kupanda miti ili kutunza mazingira na kuelezwa kwamba wanafunzi 40 wa shule hiyo walipata daraja la kwanza katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha nne, mwaka 2022.

Waziri huyo amesema Shule ya Sekondari Tumbi ni ya kwanza nchini kukabidhiwa Shilingi milioni 50, huku akiwahimiza walimu hao kuongeza juhudi zaidi ili wanafunzi wa shule hiyo wafanye vizuri katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne mwaka 2023.

“Hii ndo raha ya Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha elimu nchini, walimu wetu hawakupata fedha hii kwa upendeleo bali kwa kuchapa kazi kwa bidii,” amesema Waziri Dkt. Jafo.

Dkt. Jafo amesema shule hiyo ni mfano bora wa kuigwa nchini na shule nyingine za kata kwani imekuwa ikifanya vizuri kila mwaka na kwamba mwaka jana ilipiga hatua kubwa katika kufanya vizuri.

“Wanafunzi 40 wa Shule ya Sekondari Tumbi kupata daraja la kwanza ni jambo la kupongeza sana kwani huwezi kupata daraja la kwanza katika shule moja ya kata labda ziwe shule tatu za kata, ndio inawezekana idadi ya wanafunzi kupata daraja la kwanza kufikia 40,” amefafanua Dkt. Jafo.

Akisoma taarifa ya shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Tumbi, Bw. Fidelis Haule amesema shule yake imeweka mikakati ili kuongeza ufaulu na kwamba mwaka huu wanategemea wanafunzi 60 kupata daraja la kwanza.

Bw. Haule amesema kutokana juhudi kubwa zinazofanywa na walimu wa shule hiyo, ufaulu umekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo mwaka 2020 daraja la kwanza walipata wanafunzi 23, mwaka 2021 wanafunzi 28 walipata daraja la kwanza na mwaka 2022 walipata daraja la kwanza wanafunzi 40.

Katika hatua nyingine, Bw. Haule alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia shule hiyo shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa madarasa na maabara.

Pia Mkurugenzi wa Huduma za Elimu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Dkt. Rogers Shemwelekwa ameshukuru Serikali ya awamu ya sita kwa jitihada za kuboresha mazingira ya shule hiyo pamoja na kulipa fedha za likizo kwa walimu wa KEC.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bw. Rashid Kassim Mchatta alipongeza uongozi wa Shirika la Elimu Kibaha kwa juhudi kubwa ya kuboresha elimu katika shule hiyo.

“Shule ya Sekondari Tumbi ina kila sababu ya kufanya vizuri kwa sababu ina mazingira mazuri ya kufundishia,” amesema Bw. Mchatta.

Katika matokeo ya mwaka 2022, wanafunzi 40 wa shule hiyo walipata daraja la kwanza, 46 daraja la pili, 31 daraja la tatu, wanafunzi 36 daraja la nne na waliopata sifuri ni wanafunzi watatu tu, hivyo kufanya ufaulu kuwa asilimia 98.