Habari
DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE AMEWATAKA WANANCHI KUJENGA TABIA YA KUPIMA AFYA
DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE AMEWATAKA WANANCHI KUJENGA TABIA YA KUPIMA AFYA
- NI KATIKA MAADHIMISHO YA MIAKA HAMSINI YA CHUO CHA CHA KCOHAS
TARAHE 19/10/2018
Na Lucy Semindu SEK , Kibaha .
Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dkt. Jakaya Kikwete ameitaka jamii kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kuwahi kupata matibabu iwapo watagundulika wamepata maambukizi ya magonjwa mbali mbali.
Ameyasema hayo wakati akihutubia kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Chuo cha Sayansi Shirikishi cha Kibaha yaliyofanyika kwenye viwanja vya Tumbi Kibaha mkoani Pwani.
Alisema kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa kansa, magonjwa ya moyo, kisukari na shinikizo la damu kutokana na wahusika kugundulika wana magonjwa hayo wakiwa wamechelewa kwenda kupima afya zao.
Dkt. Kikwete alisema “iwapo tukijenga tabia ya kupima afya mara kwa mara itawasaidia kugundua tatizo walilonalo ili wapate matibabu haraka baada ya kugundulika kwa ugonjwa”.
Aidha pia Dkt. Kikwete alizungumzia tatizo la uhaba wa wauguzi, madaktari na wakunga nchini alisema pengo ni kubwa hivyo njia sahihi ya kumaliza tatizo hilo ni kuimarisha na kuvijengea uwezo vyuo vya sayansi shirikishi vilivyopo nchini ili viweze kudahili wanafunzi wengi zaidi na kuweza kumaliza tatizo la upungufu wa madaktari, wakunga na wauguzi nchini.
Hata hivyo Rais huyo wa awamu ya nne alisema kukosekana kwa wakunga na wauguzi wenye uzoefu ndio kiini cha kuendeleza vifo vya akina mama na watoto chini ya miaka mitano nchini.
Kwa hiyo aliishauri Serikali kuona namna ya kutenganisha kozi ya ukunga na uuguzi ili kupata wataalamu wenye utaalamu wa kada husika badala ya kuendelea na kuchanganya kozi hizo ambazo hupelekea ugumu wa ufanisi wa kazi yao.
Hata hiyo Dkt. Kikwete amepongeza jitihada zinazofanywa na Shirika la Elimu Kibaha katika kuimarisha sekta ya afya na elimu hasa ikizingatiwa mwaka huu Shule ya Sekondari Kibaha imekuwa ya kwanza kitaifa katika mtihani wa kidato cha sita.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Dkt. Edward Wayi alisema pamoja na changamoto zote zilizopo katika Shirika bado linaendelea kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini.
Pia aliwataka wahitimu wa chuo hicho kutumia kikamilifu elimu waliyoipata chuoni hapo katika kuwahudumia wananchi kwa kuzingatia maadili ya kazi.
Naye Mkuu wa Chuo cha Sayansi Kishirikishi cha Kibaha Dkt. Maria Manase alisema wananchi 2548 wamefanyiwa uchunguzi wa afya zao katika siku tano za maadhimisho ya chuo ya miaka 50 ya tangu kianzishwa kwa chuo hicho.
Dr. Manase aliyataja baadhi ya magonjwa yaliyokuwa yakifanyiwa uchunguzi kwa kupimwa wananchi ni kisukari, figo, afya ya koo na sikio,macho, kifua kikuu, afya ya akili, kupima virusi vya ukimwi pamoja na kuendesha uchangiaji wa adamu ambapo lita 117 za damu zimepatikana.
Mwenyekiti wa bodi ya Shirika LA Elimu Kibaha , Profesa Patrick Makungu alisema Shirika linampango wa kuanza kuzalisha viungo bandia ili kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya tano ya Uchumi wa Viwanda.