Habari
DORIS MOLLEL FOUNDATION KUPITIA VODACOM FOUNDATION YATOA MSAADA WA VIFAA VYA KUOKOA MAISHA
DORIS MOLLEL FOUNDATION KUPITIA VODACOM FOUNDATION YATOA MSAADA WA VIFAA VYA KUOKOA MAISHA YA WATOTO WACHANGA KATIKA HOSPITALI YA TUMBI
Ni vyenye thamani ya Shilingi Milioni 12
Na Lucy Semindu Kibaha – 7 Januari, 2016
Doris Mollel Foundation kupitia Vodacom Foundation leo imetoa msaada wa vifaa vya kuokoa maisha ya watoto wachanga katika Hospitali ya Tumbi vyenye thamani ya shilingi milioni 12. Akipokea msaada huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Bw. Robert Shilingi ameishukuru Doris Foundation na Vodacom kwa msaada wa vifaa walivyotoa kwa ajili ya kusaidia kuokoa maisha ya watoto wenye matatizo.
Aidha Bw. Shilingi alifafanua “kuwa ukimgusa mama na mtoto leo hii umegusa jamii”, alizipongeza taasisi zote mbili kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika maendeleo. Pia alitumia fursa hii kueleza madhumuni ya kuanzishwa kwa Shirika kupitia muasisi ambaye ni Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere ambayo ni kupambana na maadui watatu: ujinga ,maradhi na umasikini.
Kwa Upande wake mmiliki wa Doris Mollel Foundation Bi. Doris Mollel ameeleza kuwa taasisi yake imekuwa na mpango wa kusambaza zaidi ya mashine 84 za kuokoa maisha ya watoto nchi nzima kupitia wadau mbalimbali wa maendeleo.
Naye Bi Sandra Oswald ambaye ni Meneja wa Kitengo cha misaada Vodacom Foundation amesema kuwa Vodacom itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika shughuli za maendeleo.
Kitengo cha Mama na Mtoto katika Hospitali ya Tumbi kimekuwa kikijitahidi kuokoa maisha ya watoto,vifaa zaidi vinahitajika kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ili kazi hiyo iweze kufanywa kwa ufanisi zaidi.