Habari

HOSPITALI YA TUMBI YAPATIWA MSAADA WA VITANDA VYA WAGONJWA 35


HOSPITALI YA TUMBI YAPATIWA MSAADA WA VITANDA VYA WAGONJWA  35

  • Vina thamani ya zaidi ya shilingi milioni 11

Tarehe 29 MachI, 2016

Na: Lucy Semindu – Shirika la Elimu Kibaha

 Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi imepokea msaada wa vitanda vya wagonjwa 35 vyenye thamani ya zaidi ya Shiligi milioni 11 kutoka kwa Hospitali ya Kumbukumbu ya Dkt. Kariuki ya Dar es salaam. Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya Shirika la Elimu Kibaha Dkt. Peter Dattan leo katika Hospitali ya Tumbi.

Aidha Dkt. Dattan amesema msaada huo umepatikana kupitia Alumni ya MBASEA ambayo ni ya Madaktarii waliosoma Chuo cha ULM kilichopo nchini Ujerumani ambayo na yeye ni mwanachama wa Alumni hiyo. 

Alifafanua kuwa kiongozi wa Hospitali ya kumbukumbu ya Dkt. Kariuki ambaye ni mjumbe wa Alumini ya MBASEA alitangaza kuwa katika kusheherekea miaka 25 ya Hospitali hiyo wameamua watoe msaada wa vitanda 35 kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi.

Dkt Dattan amesema msaada huo umekuja wakati muafaka kwani tayari uongozi wa hospitali ulikwishabaini upungufu wa vitanda 100 ambapo wametuma maombi ya kupewa vitanda hivyo vya wagonjwa kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia ,Wazeee na Watoto.

Alibainisha kwamba vitanda hivyo vimewekwa katika wodi ya wagonjwa wa dharura za wanawake na wanaume na kwamba vitanda hivyo vyenye magurudumu vimerahisisha upelekaji wa wagonjwa kwenda kupigwa   picha ya mionzi (X- ray) inapohitajika kufanya hivyo.

Naye  Meneja wa Huduma za Uuguzi Patron. Msafiri Sehaba wa Hospitali ya Tumbi alishukuru kwa msaada huo na kwamba vile vitanda vilivyokuwa vinahitaji ukarabati sasa vitapelekwa katika karakana ya Shirika kwa ajili ya matengenezo na baadaye kuweza kutumika katika wodi nyingine zenye upungufu wa vitanda vya wagonjwa.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya  Tumbi imekuwa ni ya msaada sana kwa Mkoa wa Pwani hususan kwa kuhudumia wagonjwa wanaopata ajali za barabarani.