Habari

​Katibu Mkuu TAMISEMI awataka wahitimu kutumia fursa kukuza uchumi


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe amewataka wahitimu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC) kutumia fursa zilizopo kujiajiri ili kuongeza kipato na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla.

Hayo ameyasema leo Ijumaa tarehe 02/12/2022 alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za mahafali ya 50 ya KFDC zilizofanyika katika Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani.

“Ndugu wahitimu, leo hii mnahitimu mafunzo yenu ya miaka miwili hapa chuoni, pia wapo wale wanaohitimu mafunzo ya miezi mitatu yaliyotolewa kwa njia ya masafa ambayo yamewanufaisha wananchi wengi. Nilipopita kwenye maonesho ya fani nimeshuhudia jinsi vijana mlivyoiva kiufundi katika fani mbalimbali. Nawapongeza sana kwa kupata ujuzi katika fani hizo. Natarajia kuwa ujuzi mliopata chuoni hapa mtautumia popote mtakapo pata ajira au mtakapokuwa mmejiajiri.

“Ujuzi huu mlioupata naomba ukawasaidie kupiga hatua zaidi kimaisha. Njia rahisi ya kupata mitaji kwa sasa ni kujiunga kwenye vikundi ili kuweza kupata fedha kupitia mikopo ya asilimia kumi ya mapato kwenye kila Halmashauri ambazo hazina riba yoyote. Pia, waliopata ujuzi wa ufundi uwashi muende kuomba kazi za miradi katika Halmashauri zetu kwa kuwa mna ujuzi na vyeti, huko kuna miradi mingi ya ujenzi,” amesema Prof. Shemdoe.

Akitoa taarifa ya KFDC kwa mgeni rasmi, mkuu wa chuo hicho, Bw. Joseph Nchimbi ameeleza kuwa chuo hicho kinatoa mafunzo ya fani za ujuzi wa aina mbalimbali, kina jumla ya wanachuo 383 wa kozi ndefu wakiwemo 235 mwaka wa kwanza na 170 mwaka wa pili.

“Chuo kimefanikiwa kuanzisha kozi fupi zaidi ya kumi ambazo zinatolewa kwa njia ya kiswahili na kuwafikia idadi kubwa ya wanufaika kwa wakati mmoja,” alisema Bw. Nchimbi.

“Tumefanikiwa kutoa mafunzo ya nadharia na vitendo kwa wanafunzi wa muda mrefu na muda mfupi, na wameendelea kufanya vizuri katika mitihani yao ya VETA. Wahitimu wetu wameweza kupata ajira katika taasisi mbalimbali na kujiajiri pia,” alisema Bw. Nchimbi.

“Fani zinazotolewa na KFDC ni ufundi bomba; ufundi wa umeme majumbani; ufundi wa magari; ufundi wa uungaji na uundaji vyuma; ufundi wa uwashi; ufundi wa useremala; ufundi wa ushonaji nguo na ubunifu wa mavazi; kilimo cha bustani na mazao mbalimbali; ufugaji; hotelia na udereva,” alisema Bw. Nchimbi.

Mahafali hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Halmashauri ya Mji Kibaha, Shirika la Elimu Kibaha, Mamlaka ya Elimu Tanzania, Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Shirika lisilo la kiserikali la Karibu Tanzania, viongozi wa dini, wahitimu, ndugu na wazazi wa wahitimu na waandishi wa habari.