Habari

​KEC yapongezwa kwa kutekeleza vyema Ilani ya CCM


Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mjini, Bi. Mwajuma Nyamka leo Alhamisi tarehe 07/09/2023 amelipongeza Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kwa kutekeleza vyema ilani ya CCM.

Pongezi hizo zimetolewa baada ya Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kibaha Mjini ikiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini kutembelea, kukagua na kuridhishwa na mradi wa ujenzi wa darasa moja katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha (KCOHAS) lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 100 kwa wakati mmoja.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Kaimu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha (KCOHAS) Bw. Said Kondo ameeleza kuwa KCOHAS ni chuo kilichopo chini ya Shirika la Elimu Kibaha na kilianzishwa mwaka 1963 kwa lengo la kupambana na adui maradhi huku kikitoa mafunzo ya utabibu na uuguzi na ukunga kwa ngazi ya stashahada.

“Ujenzi wa darasa hili kubwa ulianza Januari 2022 na kukamilika Disemba 2022 na kugharimu kiasi cha Tsh. 56,849,224.36 zikiwa ni fedha za mapato ya ndani ya KEC kwa lengo la kutoa elimu na mafunzo kwa wanafunzi wengi zaidi kwa wakati mmoja," amesema Bw. Kondo.

Akizungumza katika ziara hiyo, Bi. Nyamka amewapongeza KEC kwa kuwa wabunifu na kujitoa kuhakikisha huduma ya elimu ya afya inawafikia vijana wengi wa kitanzania ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM).

“Tunawapongeza sana kwa kuwa wabunifu na kujiongeza mbali na vyanzo vyenu vya mapato kupungua bado mmeweza kujibana na kujenga darasa kubwa kama hili, hongereni sana kwa utekelezaji wa ilani ya CCM na hivi ndivyo inavyotakiwa, alisema Bi. Nyamka, Mwenyekiti CCM Wilaya ya Kibaha Mjini.

Ziara hiyo ya Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kibaha Mjini pia ilihudhuriwa na Katibu wa CCM Wilaya ya Kibaha Mjini, Katibu Tawala wa Wilaya ya Kibaha, Viongozi wa CCM tawi la Tumbi, Viongozi wa CCM Kata ya Tumbi, wajumbe wa baraza la Maendeleo ya Kata ya Tumbi, wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Kibaha, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa KEC Bw. Anathe Nnko na timu ya menejimenti ya KEC.