Habari

​Kurugenzi ya Elimu yapongezwa kuanzisha kikao kazi cha kujitathimini


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Bw. Anathe Nnko leo tarehe 30/11/2023 ameipongeza kurugenzi ya elimu kwa kuanzisha kikao kazi cha kujitathimini ili kuwezesha jamii kupata huduma bora.

Bw. Nnko amewaelekeza walimu kuhakikisha wanatoa huduma bora kulingana na fani zao ili Shirika la Elimu Kibaha liweze kufikia malengo.

“Nawaomba watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha kushirikiana kwa vitendo na siyo kwa maneno ili kuwawezesha wanafunzi kupata elimu bora,” amesema Mkurugenzi Nnko.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Elimu wa Shirika la Elimu Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa amesema Shirika la Elimu Kibaha ni Shirika kiongozi kwenye elimu kwani kila mwaka shirika hili limekuwa likipata matokeo mazuri katika mitihani mbalimbali.

Vilevile, Dkt. Shemwelekwa amemshukuru Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii, Bw. Anathe Nnko kwa kusaidia kufundisha somo la kilimo katika Shule ya Sekondari Kibaha.

“Mwakani na mimi nitaanza kuingia darasani kufundisha somo la hisabati, kwa njia hii tutaleta matokeo mazuri kwenye shule zetu,” amesema Dkt. Shemwelekwa.

Naye Bw. Khalfan Feruzi kwa niaba ya Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala, Shirika la Elimu Kibaha ameipongeza Kurugenzi ya Elimu kwa matokeo mazuri ya darasa la saba shule ya msingi Tumbi lakini pia ametumia kikao hicho kutoa elimu kuhususiana na kanuni na sheria za kiutumishi ili kuwakumbusha watumishi walimu na wasio walimu haki na wajibu wao wawapo kazini.

Katika kikao hicho, mada mbalimbali zilijadiliwa zikiwemo maadili na maslahi ya watumishi wa umma, utekelezaji wa kazi za Januari hadi Disemba 2023 kutoka kwenye vitengo, mpango wa kuhuisha shughuli za kurugenzi na mpango wa masuala ya kijamii katika kurugenzi ya elimu.