Habari

Maafisa KEC wapatiwa mafunzo ya kuandaa bajeti


Maafisa bajeti wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) leo Jumanne tarehe 16/11/2022 wamepatiwa mafunzo kuhusu uandaaji wa bajeti katika mwaka wa fedha 2023/2024; taarifa za utekelezaji wa bajeti za kila robo mwaka na mipango mikakati ya utekelezaji wa shughuli za kurugenzi na vitengo vyao.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Eimu Kibaha (KEC), Bw. Robert Shilingi amewataka maafisa hao kufuatilia kwa makini mafunzo hayo ili kuandaa bajeti za Shirika ambazo italeta maendeleo katika Shirika hilo.

“Muwe makini katika kuandaa bajeti ambazo zitakuwa na uhalisia ili kuwezesha uendeshaji mzuri wa taasisi yetu. Mmeaminiwa na kurugenzi na vitengo vyenu, hivyo ni yema kuzingatia mahitaji yote yanayotakiwa. Niwatakie kila la kheri kwenye mafunzo yenu,” amesema Bw. Shilingi.

Akiwasilisha mada katika mafunzo hayo, mkufunzi wa mafunzo hayo Bw. Stephano Mbena amewasisitiza maafisa bajeti kufahamu mambo yote ili kuandaa bajeti nzuri inayotekelezeka.

“Sehemu kubwa ya Bajeti inaangalia sheria, hivyo ni muhimu kuzingatia mwongozo wa bajeti kwa mwaka wa fedha husika bila kusahau ilani ya Chama Tawala, sera ya bajeti, mpango wa matumizi ya Serikali na mpango mkakati wa miaka mitano,” amesema Bw. Mbena.

Mafunzo hayo ambayo yameandaliwa na Kitengo cha Mipango, Tathimini na Ufuatiliaji cha Shirika la Elimu Kibaha (KEC), yanafanyika kwa siku tatu kuanzia leo tarehe 16/11/2022 hadi tarehe 18/11/2022 na yanalenga kujenga uelewa kwa maafisa hao juu ya kuandaa bajeti, malengo mahususi na shughuli zitakazotekelezwa na taasisi kufikia malengo hayo; kuandaa maombi maalum na matumizi ya mfumo wa kuandaa na kutolea taarifa za hatua za utekelezaji wa bajeti (Planrep) na uandaaji wa taarifa za utekelezaji wa shughuli za Shirika (KEC) za kila robo mwaka na mipango mikakati ya kufikia malengo ya taasisi.