Habari

MADAKTARI WANAFUNZI WA UDOM WACHANGIA DAMU KWA AJILI YA HOSPITALI YA TUMBI


MADAKTARI WANAFUNZI WA UDOM WACHANGIA DAMU KWA AJILI YA HOSPITALI YA TUMBI

 Tarehe 31 Julai, 2016

Madaktari wanafunzi wa UDOM wachangia damu kwa ajili ya hospitali ya Tumbi. Tukio hilo la msaada wa kibinadamu limefanyika mwisho wa wiki iliyopita katika Kitengo cha damu salama cha Hospitali ya Tumbi.

Akiwashukuru Madaktari wananafunzi hao, Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Afya Shirika la Elimu Kibaha ambaye pia ni Daktari Bingwa wa mifupa, Dkt. Brycson Kiwelu amesema katika kipindi cha miaka mitatu alichokaa shirikani ni kwa mara ya kwanza ameshuhudia madaktari wanafunzi wakijitolea damu.

Aliwapongeza sana kwa hatua hiyo ya kujitolea damu na amesema damu waliojitolea itasaidia sana kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji wa damu. Pia aliwataka muungano huo walioonesha uendelee kwa kufanya mambo mengine kwa pamoja kama vile kuanzisha Hospitali ili waweze kujiajiri.

Awali akielezea kazi za Kitengo cha Damu Salama cha Hospitali ya Tumbi, Mkuu wa Kitengo hicho Sister Elisia Towo amesema kitengo kinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuwezesha wachangia damu kuchangia kwa ajili ya watu wenye uhitaji mkubwa damu.