Habari

MAKABIDHIANO YA MASHINE YA X-RAY KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA PWANI TUMBI


TAARIFA KWA VYOMBO  VYA HABARI

MAKABIDHIANO YA MASHINE YA X-RAY KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA PWANI  TUMBI

Kibaha ,Septemba 27,2019

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi imekabidhiwa  na mgeni rasmi Mkuu wa Mkoa wa Pwani vifaa tiba vinavyojumuisha mashine ya X-ray na Mashine ya Ultra Sound vilivyotolewa na wahisani KOFIH kutoka nchini Korea.

Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Gunini Kamba amesema vifaa hivyo vimekuja wakati muafaka kwani mashine ya X- Ray iliyopo ina zaidi ya miaka 20 na kwamba ujio wa mashine hii ya kidigitali ni mkombozi kwani itafanya kazi kwa haraka zaidi na kuhifadhi kumbukumbu .

Dkt.Gunini Kamba kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Enjinia Evarist Ndikilo ameishukuru Serikali ya Korea Kusini kupitia KOFIH ambalo ni Shirika linalojihusisha na maendeleo ya afya ya mama na mtoto kutoka Korea Kusini. Amesisitiza matumizi bora ya vifaa hivyo ili viweze kutumika kwa muda mrefu zaidi na kuweza kuhudumia wagonjwa wanaoletwa katika Hospitali ya Tumbi.

Awali akitambalulisha ushirikiano kati ya KOFIH na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Tumbi Mkurugenzi wa huduma za Afya Shirika la Elimu Kibaha  Dkt. Edward Wayi amesema ushirikiano huu umeanza tangu mwaka 2009 na umelenga kuhudumia Mama na mtoto.

Akitoa maelezo ya kina kuhusu ushirikiano huo  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Dkt. Robert Shilingi amesema msaada wa ushirikiano umejumuisha ununuzi wa mashine ya X-ray uliogharimu kiasi cha milioni 420,000,000 na mashine ya Ultra Sound iliyogharimu dola za kimarekani 20,000 na hivyo kufanya gharama ya vifaa hivyo kufikia shilingi milioni 500,000,000. Bw. Shilingi amesema ushirikiano huu umeleta manufaa makubwa na umehusisha Ujenzi wa jengo la radiolajia ambalo lina  chumba cha upasuaji cha kina mama,ukarabati wa jengo la mama na mtoto,mafunzo ya wataalam mbalimbali ikiwemo vifaa tiba na usingizi pamoja na utoaji wa elimu ya matengenezo ya vifaa tiba katika Hospitali ya Tumbi.

Ameishukuru KOFIH kwa msaada huo na kwamba vifaa hivyo vitatunzwa ili viweze kuleta tija iliyokusudiwa.Pia amesema mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya tano ni pamoja na kupunguza uhaba wa Madaktari kutoka 48% mwaka 2016 na kufikia 33% mwaka 2019,ongezeko la Madaktari Bingwa kutoka 9 hadi kufikia madaktari 15. Uendelezaji wa miundo mbinu na upanuzi wa Hospitali ya Tumbi.

Sanjari na hilo amesema kumekuwa na mafanikio katika ukusanyaji wa mapato ambayo imetokana na matumizi ya mfumo mpya wa ukusanyaji mapato ya Serikali wa kielektroniki wa GEPG kwani takwimu zinaonesha katika kipindi cha miezi mitatu katika hospitali ya Tumbi zimepatikana shilingi 209,000,000 wakati kwa kipindi kama hicho kabla ya kutumia mfumo huo zilipatikana shilingi 190,000,000.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bw Shilingi pia ametaja miradi inayotarajiwa kujengwa ni pamoja na ujenzi wa chumba maalum cha uangalizi cha watoto pamoja na ujenzi wa Kituo cha kuhudumia walioathirika na matumizi ya madawa ya kulevya.

Naye Mwakilishi mkazi wa KOFIH Dkt. Wonkyu Woo amesema ushirikiano wa Shirika lake na Hospitali ya Tumbi una miaka kumi sasa. Wakati Mkurugenzi wa KOFIH Korea  Dkt. Kim Hyun Kyong amesema ameanza kuja nchini Tanzania kutoa huduma na kibinadamu tangu miaka 20 iliyopita wakati huo kwenye kambi ya wakimbizi ya Ngara na kwamba kwa sasa yeye kama Mkurugenzi wa KOFIH wataendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa misaada katika Hospitali mbalimbali nchini. 

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi imekuwa ikihudumia wagonjwa mbalimbali na hasa wanaopata ajali za barabarani na imekuwa ikitoa huduma bora na kwa haraka kwa majeruhi wa ajali za barabarani na viwandani.