Habari

​Makamu wa Rais awazawadia walimu Shule ya Sekondari Tumbi Shilingi milioni 50


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango amewapongeza walimu wa Shule ya Sekondari Tumbi inayomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha (KEC) mkoani Pwani sambamba na kuagiza walimu hao kupewa Shilingi milioni 50 kwa kufaulisha vizuri katika mtihani wa Taifa wa kidato cha nne uliofanyika mwaka jana.

Juhudi za walimu wa Shule ya Sekondari Tumbi imemvutia Mhe. Dkt. Mpango na kumuagiza Waziri wa Nchi, Ofizi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Said Jafo kuwapatia walimu hao shilingi milioni 50 ikiwa ni motisha baada ya wanafunzi wa shule hiyo kufanya vizuri.

Katika mtihani huo, wanafunzi 40 walifaulu katika ngazi ya daraja la kwanza, 46 daraja la pili, 31 daraja la tatu na wanafunzi 36 daraja la nne na waliopata ziro ni wanafunzi watatu, hivyo kufanya ufaulu kuwa asilimia 98.

Shule hiyo ambayo inasimamiwa na Mwalimu Mkuu, Bw. Fidelis Haule imekuwa ikifanya vizuri katika kipindi cha miaka saba mfulilizo katika mitihani ya Taifa ya kidato cha nne.

Akizungumza leo tarehe 04/02/2023 baada ya kuongoza shughuli ya upandaji wa miti shuleni hapo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 46 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mhe. Dkt. Mpango amesema fedha hizo ni motisha kwa walimu 50 wanaofundisha katika Shule hiyo.

"Nakuagiza Waziri Selemani Jafo (Waziri wa Nchi, Ofizi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mhe. Dkt. Selemani Said Jafo) watafutie walimu hawa Shilingi milioni 50, waletee hizo fedha walimu," amesema Mhe. Dkt. Mpango katika ziara ya siku moja ya kuadhimisha miaka 46 ya CCM.

Awali, akitoa taarifa ya taaluma katika shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Tumbi, Fidelis Haule amesema tangu akabidhiwe kuingoza Shule hiyo miaka saba iliyopita kumekuwa na matokeo mazuri kila mwaka.

Amesema mbinu inayowawezeha kufaulisha vizuri kila mwaka, ni juhudi za kufundisha kwa ushirikiano wa pamoja bila kujali hali ya mwanafunzi anakotoka.

Katika hatua nyingine, mwanafunzi Neema Baraka Shuma alimweleza Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Mpango kuwa shule hiyo ina walimu wa kutosha na mazingira mazuri ya kusomea.

"Hatuna changamoto yoyote shuleni kwetu, hapa tuna walimu wazuri, pia majengo ya shule yetu yanaendelea kukarabatiwa, hivyo tunaishukuru Serikali kwa kutujali,” amesema Neema Baraka Shuma.

Makamu huyo wa Rais amewataka walimu na wanafunzi wa shule hiyo kuongeza juhudi ya utunzaji wa mazingira ili kulinda vyanzo vya mvua na kuepuka majanga mbalimbali.