Habari

Mbunge aahidi kutatua changamoto Kibaha Sekondari


Mbunge wa jimbo la Kibaha mjini Bw. SylvestryKoka ameahidi kushirikiana na uongozi wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) pamoja na shule ya sekondari Kibaha kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kutengeneza mazingira mazuri ya kujifunzia.

Hayo ameyasema leo Alhamisitarehe 27/10/2022 akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 56 ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Kibaha baada ya kusikiliza na kupokea risala ya wanafunzi wahitimu na taarifa ya shule hiyo.

“Shule imekuwa ikifanya vizuri katika mitihani ya Taifa ya kidato cha nne na cha sita. Ufaulu wa shule yetu kwa kidato cha nne ni asilimia 100 tangu mwaka 2015 hadi 2021. Na matarajio ya mwaka huu 2022 kwa wahitimu wa kidato cha nne ni shule kuwa katika kumi bora kitaifa.” Amesema Bw. Jonas Mtangi, kaimu mkuu wa shule ya sekondari Kibaha akitoa taarifa ya shule kwa mgeni rasmi.

“Changamoto kubwa zinazoikabili shule yetu ni ukosefu wa kisima kikubwa cha kuhifadhia maji; upungufu wa vifaa vya maabara ya kompyuta; uchakavu wa majiko makubwa ya gesi ya kupikia na upungufu wa samani za bwalo la kulia chakula.” Amesema Bw. Innocent Kaaya, mwanafunzi wa kidato cha nne, akisoma risala ya wahitimu kwa mgeni rasmi.

Akijibu risala hiyo, Mhe. Koka ameahidi ofisi yake kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto hizo na kuwataka wazazi na wadau wengine kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuweka mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia.

“Ofisi ya mbunge itashirikiana na Mkurugenzi Mkuu wa KEC pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari Kibaha kutatua changamoto nilizozipokea. Nawasihi ndugu zangu, jukumu la kusimamia maendeleo katika elimu si la Serikali pekee, nawaomba wadau wote mkiwemo wazazi kutuunga mkono katika kufanikisha maendeleo mbalimbali ya shule yetu kwa kujitolea kwa hali na mali.” Amesema Mhe. Koka.

Mhe. Koka pia amechukua nafasi hiyo kuwapongeza wahitimu hao na kuwaasa kusoma kwa bidii ili kufanya vizuri katika mtihani wao wa taifa. Aidha amewataka kuwa waadilifu kwenye jamii na kutumia ujuzi wao kwa maendeleo yao binafsi na taifa kwa ujumla.

“Nawapongeza kidato cha nne kwa kuhitimu masomo yenu, haya yote mtayafanikisha kama mtaendeleza nidhamu na kujituma. Kusoma kwenu kwa bidii kunawapa wigo mkubwa wa kuchagua taaluma yoyote kwa siku zenu za usoni na hatimaye tupate wataalamu na viongozi wakubwa katika taifa letu.”Amesema Mhe. Koka

Katika mahafali hayo, Mhe. Koka kwa kushirikiana na wazazi waliweza kuchangia Tsh. 1,865,000 kuunga mkono maendeleo ya shule hiyo.

Mahafali hayo yaliyohusisha wanafunzi wahitimu 91, yamefanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Kibaha inayomilikiwa na Shirika la Elimu Kibaha yakihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa KEC Bw. Robert Shilingi, viongozi wa bodi ya shule hiyo, menejimenti ya KEC, walimu, wazazi na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kibaha na Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha.