Habari

Mbunge Kibaha Mjini atembelea miradi ya maendeleo Shirika la Elimu Kibaha


Mbunge wa Kibaha Mjini, Mhe. Sylvestry Francis Koka, jana tarehe 01/11/2021, amefanya ziara na kutembelea miradi miwili ya maendeleo inayotekelezwa na Shirika la Elimu Kibaha.

Mhe. Koka ametembelea na kuona maendeleo ya ujenzi wa mabweni matatu (3) katika shule ya Wasichana Kibaha yaliyoletewa Tsh. 240,000,000/= ambapo kila bweni linagharimu Tsh. 80,000,000/= na ukarabati wa majengo ya shule na ujenzi wa madarasa matatu (3) katika shule ya msingi Tumbi wenye jumla ya Tsh. 281,805,829/=. Fedha zote zimetoka Serikali kuu chini ya mpango wa EP4R.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Koka amewataka wataalam kusimamia vyema ujenzi huo na kutafuta fedha kwenye vyanzo vingine ili kukamilisha mabweni yote matatu na yaanze kutumiwa na wanafunzi.

"Kwa kuwa fedha iliyoletwa kwa ujenzi wa mabweni haya matatu, katika utekelezaji inaonyesha haitatosha kukamilisha majengo haya na wanafunzi wakaanza kuyatumia, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha na wataalam wako tunatakiwa kujengea hoja swala hili tupate fedha za kumalizia majengo haya". Alisema Mhe. Koka.

Ziara hiyo ilikuwa maalum kwa Mhe. Koka kukagua miradi inayotekelezwa katika jimbo lake na ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Ndg. Robert Shilingi, Wakurugenzi wa kurugenzi na vitengo kutoaka Shirika la Elimu Kibaha.