Habari

MFUMO WA GOT- HOMIS WAONESHA MAFANIKIO KATIKA UKUSANYAJI MAPATO


MFUMO WA GOT- HOMIS WAONESHA MAFANIKIO KATIKA UKUSANYAJI MAPATO

Na: Lucy Semindu  - Kibaha

Mfumo wa Got-Homis waonesha mafanikio katika ukusanyaji mapato hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Dkt. Cyprian Mpemba wakati wa kikao cha wadau wa mfumo huo wa hospitali kilichofanyika jana katika ukumbi wa Bertil Merlin wa Shirika la Elimu Kibaha.

Dkt. Cyprian Mpemba amesema  mfumo wa Got-homis umeingia katika hatua ya pili ambapo kwa sasa utaanza  kutumika kupitia  kadi  bila kulipa pesa taslim   (cashless)   kwa ushirikiano na  benki ya NMB .

Aidha, Dkt. Mpemba alifafanua kuwa mfumo wa Got-homis uliobuniwa na Shirika la Elimu Kibaha mwaka 2014 kwa sasa umeshafungwa katika hospitali za Mikoa, Wilaya na vituo vya afya zaidi ya 54 nchini. Mfumo huo umeonesha mafanikio makubwa katika ukusanyaji mapato ya hospitali kuliko ilivyokuwa hapo awali kabla ya kuanza kutumika kwa  mfumo huo.

Akielezea namna mfumo huo unavyofanya kazi mmoja wa waratibu wa mfumo huo bwana Joseph Mnyala amesema mfumo huo ambao kwa sasa utamwezesha mteja kutumia Afya card anapotaka kupatiwa huduma katika hospitali yoyote yenye mfumo wa Got-homis . Mteja  ataweka pesa kwenye Afya card  kupitia   Mpesa , na NMB mobile.

Shirika la Elimu Kibaha kwa sasa imeshaingia kwenye makubaliano na NMB na Mpesa mazugumzo yanaenedelea na kampuni nyingine za simu ili kadi hiyo iweze kutumika kupitia kampuni hizo pia.

Mfumo huo pia utasaidia taarifa za mgonjwa kupatikana kirahisi ,daktari ataweza kumwandikia mgonjwa vipimo na dawa .Pia mgonjwa akiwa na mzio (allergy) ya dawa fulani ataandikwa ili mgonjwa huyo asiandikiwe dawa hiyo kwa usalama wa maisha yake.