Habari
Mhe. Bashungwa alitaka Shirika la Elimu Kibaha kuwasaidia wahitimu wa vyuo na sekondari kupata ajira
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). Mhe. Innocent Bashungwa amelitaka Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kutoa mafunzo yatakayowasaidia wahitimu wa sekondari na vyuo kupata ajira.
Kauli hiyo imetolewa na Mhe. Bashungwa baada ya kutembelea shirika hilo kukagua miradi ya elimu ya ujenzi wa mabweni, madarasa pamoja na ukarabati wa shule za shirika hilo ambayo inatekelezwa kwa fedha za Serikali.
Miradi inayosimamiwa na shirika hilo ni ujenzi wa mabweni na madarasa katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha, Ujenzi wa madarasa katika Shule ya Sekondari Tumbi, ukarabati wa madarasa na ujenzi wa madarasa mapya katika Shule ya Msingi Tumbi na ujenzi wa jengo la kujifunzia katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Kibaha.
Katika kikao cha kuhitimisha ziara hiyo, Waziri wa TAMISEMI, Mhe. Bashungwa aliagiza uongozi wa shirika kuanzisha mafunzo ya muda mfupi ambayo yatawasaidia wahitimu kujiari.
Katika hatua nyingine, Waziri amesema Serikali ya awamu ya sita itaangalia uwezekano wa kuanza ujenzi wa nyumba za walimu ili kuondokana na kero hiyo.
“Nitazungumza na Halmashauri ili watenge fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu,” amesema Mhe. Bashungwa.
Pia, baada ya kutembelea miradi ya ujenzi na ukarabati wa madarasa, Waziri amesema ameridhishwa na menejimenti ya shirika kwa kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa miradi hiyo.
Naye, MKurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Robert Shilingi akitoa historia fupi ya shirika hilo kwa Mhe. Bashungwa, amesema KEC inatoa elimu ya sekondari, msingi, shughuli za kilimo, ufugaji na kutoa mafunzo kwa maofisa tabibu.
Mkurugenzi huyo vile vile, ameishukuru Serikali kwa kulipatia shirika hilo fedha za ujenzi na ukarabati wa shule hizo.