Habari

Miradi ya Maendeleo KEC yamvutia Mkurugenzi wa Sera, Mipango wa Wizara ya Elimu


Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Bw. Atupele Mwambene leo tarehe 20/12/2022 ametembelea Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ili kuona na kupokea taarifa ya miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Shirika.

Bw. Mwambene ametembelea mradi wa ujenzi wa jengo-mseto ambalo litatumika kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao (online), ukarabati wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC) na ujenzi wa mabweni katika Shule ya Sekondari Wasichana Kibaha.

Akimkaribisha Bw. Mwambene, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Bi. Chiku Wahady ameeleza kuwa Shirika lina mkakati wa kuboresha huduma za elimu ikiwa ni pamoja na kuibua miradi mipya ya kutoa mafunzo ya ujuzi kwa wananchi.

Naye, Mkurugenzi wa Huduma za Elimu wa KEC, Dkt. Rogers Shemwelekwa amesema Shirika lina mpango wa kujenga shule ya msingi ya ufundi ambayo itatumia lugha ya kiingereza sambamba na kuanzisha kituo cha michezo ‘sports academy’ ambayo ni sehemu ya mradi huo kwa lengo kuwawezesha wanafunzi kuwa chachu ya kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Vile vile amemweleza Bw. Mwambene kuwa KEC imeshaanza ujenzi wa jengo-mseto lenye miundombinu ya TEHAMA kwa ajili ya kutoa elimu kwa njia ya masafa ili kukabiliana na ukosefu wa walimu nchini katika baadhi ya masomo.

“Wakati mwalimu anafundisha kupitia jengo-mseto hapa Kibaha, basi wanafunzi walioko sehemu mbalimbali nchini wanaweza kufuatilia vipindi na kuuliza maswali kupitia mtandao (online),” amesema Dkt. Shemwelekwa.

Dkt. Shemwelekwa vile vile amempatia Bw. Mwambene taarifa ya ukarabati wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha (KFDC) ili kuongeza udahili wa wanafunzi kutoka 400 hadi 800.

Baada ya Bw. Mwambene kupokea taarifa ya miradi hiyo, ameahidi kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi hiyo ili kuliwezesha Shirika la Elimu Kibaha kuongeza wigo wa shughuli zake pamoja na kuwafikia wananchi.