Habari

MKUU WA MKOA MHE. EVARIST NDIKILO ASIFU JUHUDI ZINAZOFANYWA NA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA KATIKA KUPAMBANA NA UJINGA, MARADHI NA UMASIKNI


Mkuu wa Mkoa mpya wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Evarist Ndikilo amesifu juhudi zinazofanywa na Shirika la Elimu Kibaha katika Kupambana na maadui watatu ambao ni Ujinga,maradhi na Umasikini.

Mhe. Ndikilo ameyasema hayo katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha kabla ya kukutana na wafanyakazi wa Halmashauri ya Kibaha mji,wilaya na wa Shirika la Elimu katika Ukumbi wa B. Merlin.

Aidha,Mhe Ndikilo amesema kuwa anatambua kuwa   Shirika kwa sasa lina miaka zaidi ya hamsini na lipo likiendelea na shughuli za kutoa huduma kwa jamii inayoizunguka. Pia amesema anatambua juhudi zinazoelekezwa na Shirika la Elimu Kibaha katika maendeleo ya elimu na kwamba Kibaha Sekondari ni kielelezo cha mafanikio hayo.

Awali akitoa maelezo mafupi ya maendeleo ya Shirika, Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha Dk. Cyprian Mpemba  amesema kuwa kwa sasa Shirika lina miaka  zaidi ya hamsini na linaendelea kutekeleza misingi mikubwa ya  kuanzishwa kwa Shirika .

Ametaja misingi hiyo ni kupambana na ujinga ,maradhi na umasikini, kwa kuanzisha Shule kuanzia Chekechea hadi Sekondari, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi ili Vijana na Wakulima wapate mafunzo ya kuwasaidia kupambana na umasikini na hospitali ya Tumbi ili kupambana na maradhi ikiwemo Chuo cha utabibu.

Aidha, DK.Cyprian Mpemba amesema kuwa jana Hospitali ya Tumbi imeanza kuhudumia wagonjwa katika wodi ya wagonjwa mahututi ICU na kwamba kuanza kwa huduma hiyo ni mafanikio makubwa kwa Shirika la Elimu Kibaha.

Akiongea na watumishi wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Ndikilo amesema anatambua juhudi kubwa inayofanywa na watumishi wa Kibaha katika kuleta maendeleo na hivyo ipo haja ya kuendelea kutoa huduma bora na kwa uadilifu mkubwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Hajat Halima Kihemba amesifu ziara ya Mkuu wa Pwani ya  kukagua miradi ya maendeleo. Mhe. Kihemba  amesema mafanikio yaliyopatikana katika Wilaya yake yametokana na ushirikiano na Juhudi za kila mmoja yaani; Watumishi Madiwani, Wadau na Wananchi kwa ujumla.