Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Shirika La Elimu Kibaha

ZAIDI YA WANANCHI 1,000 WAPATA TAARIFA ZA SHIRIKA.

Imewekwa: 22 Aug, 2025
ZAIDI YA WANANCHI 1,000 WAPATA TAARIFA ZA SHIRIKA.

Wananchi zaidi ya 1,000 wamejitokeza katika Maonesho ya Wakulima ya Nanenane mwaka 2025 jijini Dodoma ambayo yalihitimishwa tarehe 10/08/2025 kwenye Viwanja vya John Malecela jijini Dodoma.

Maonesho hayo yalianza tarehe 01 hadi 10, 2025 kwenye viwanja hivyo ambako wakulima, taasisi za umma na  taasisi binafsi zilishiriki na kutoa huduma na kuonesha bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na wakulima pamoja na wataalamu.

Katika Banda la Shirika la Elimu Kibaha, wananchi walipatiwa maelezo kuhusu Shirika na jinsi linavyosimamia utoaji wa elimu ya sekondari na msingi kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Pia, wananchi walielezwa kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika la Elimu Kibaha ambazo ni utoaji wa elimu ya msingi na sekondari.

Katika maonesho hayo, pia wananchi wakiwemo wanafunzi wa shule za sekondari na msingi walielezwa kwamba Shirika lina vyuo viwili; Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha ambacho kinatoa mafunzo ya ufundi wa magari, ufundi bomba, ufundi umeme wa majumbani, ufundi uundaji na uungaji vyuma, ufundi ujenzi, ufundi seremala, ufundi ushonaji wa mavazi na ubunifu wa mitindo, stadi za maisha na udereva, upishi, ufugaji na kilimo.

Wananchi, pia walipewa maelezo ya kozi zinazotolewa na Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha ikiwemo kazi ya stashahada ya utabibu, stashahada ya uuguzi na ukunga na astashahada ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Banda la Shirika la Elimu Kibaha, lilitembelewa na wananchi kutoka Dodoma, Morogoro, Kilimanjaro, Dar es Salaam, Tabora, Iringa, Arusha,Singida na Mbeya.