Habari

​Rais Mstaafu Jakaya Kikwete atembelea banda la maonesho la Shirika la Elimu Kibaha


Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muunganiko wa Tanzania awamu ya nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete leo Alhamisi tarehe 06/10/2022 ametembelea banda la maonesho la Shirika la Elimu Kibaha katika maonesho ya Biashara na Uwekezaji yanayofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani ya mailimoja Kibaha, Mkoa wa Pwani.

Mhe. Kikwete ametumia nafasi hiyo kusisitiza Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha ili kuhimili ushindani wa soko.

"Mnapotengeneza bidhaa zenu, hakikisheni mnazingatia ubora kwa kulenga soko la ndani na la nje ya nchi." Amesema Mhe. Kikwete.

Mhe. Kikwete pia amelipongeza Shirika la Elimu Kibaha kwa kuendelea kutoa elimu kwa vitendo kulingana na mahitaji ya teknolojia ya sasa.

"Mashine hizi mnazotengeneza zinasaidia kurahisisha shughuli za kilimo, ila mjitahidi kuzingatia ubora wake ili kuhimili ushindani wa soko uliopo," amesema Mhe. Kikwete.

Mhe. Kikwete pia amevitaka vyuo vyetu vijipange vizuri kutoa mafunzo ya ujuzi unaoendana na soko la ajira lililopo.

"Angalieni aina ya viwanda kwenye Mkoa wenu, na zingatieni elimu mnayoitoa iendane na viwanda mlivyonavyo ili kuwapatia nafasi kwenye soko la ajira wahitimu wa vyuo hivyo". Amesema Mhe. Kikwete.

Mhe. Kikwete ni mgeni rasmi wa maonesho hayo ya Biashara na Uwekezaji Mkoa wa Pwani ambayo

yanafanyika katika viwanja vya stendi ya zamani ya mailimoja yakilenga kuvutia wawekezaji kwa kuonyesha huduma na fursa zilizopo kwenye Mkoa wa Pwani.