Habari

​Shirika la Elimu Kibaha latakiwa kutoa elimu ya kuwawezesha wananchi kujiajiri


Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Charles Msonde ametembelea Shirika la Elimu Kibaha na kuwataka watumishi kubadilika na kuonyesha utofauti uliopo kwenye latakiwa huduma wanazotoa ukilinganisha na maeneo mengine.

Akizungumza na wajumbe wa menejimenti ya Shirika la Elimu Kibaha, Dkt. Msonde amelitaka Shirika la Elimu Kibaha kuonyesha utofauti ulilonalo kwa kutekeleza malengo ya uanzishwaji wake kwa utofauti na maeneo mengine.

“Lazima tuangalie kwa namna gani Shirika la Elimu Kibaha tangu kuanzishwa kwake limeweza kutatua changamoto zilizofanya lianzishwe yaani umasikini, maradhi na ujinga.”

“Taasisi zilizo chini ya Shirika zipo pia sehemu nyingine, hivyo ni lazima Shirika muonyeshe utofauti mlio nao na taasisi nyingine.”

Dkt. Msonde pia ameagiza Shirika la Elimu Kibaha kubadilisha taratibu za utekelezaji wa majukumu yake na kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa elimu ya kupata ujuzi zaidi katika kutatua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye jamii.

“Lazima shule zetu na vyuo vyetu viwe na utaratibu tofauti, nataka vyuo na shule za kupata ujuzi. Tuwe na miradi ya kutuondolea umasikini kwa watu wetu. Tuwe na vitu ambavyo vitawafanya watu wapate ujuzi wa kujiajiri na kutatua changamoto zilizopo katika maisha ya kawaida.

Pia Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Robert Shilingi alitumia nafasi hiyo kueleza malengo ya utendaji kazi wa Shirika na malengo waliyojiwekea kutekeleza.

“Kulingana na waasisi wa Shirika hili, Shirika letu limejikita katika kutoa elimu ili kupambana na maadui watatu ambao ni ujinga, maradhi na umasikini. Utekelezaji wa majUkumu yetu unafanyika kupitia taasisi zilizo chini ya Shirika ambazo ni Shule ya watoto wadogo Tumbi; Shule ya Msingi Tumbi; Shule za Sekondari Kibaha, Tumbi na Kibaha Wasichana; Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha.”

“Shirika hili ni la kutoa huduma, ila tuna mpango wa kuanza kuzalisha ili tuweze kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya uendeshaji wa Shirika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.” Alisema Bw. Shilingi.

Ziara ya Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Charles Msonde ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake katika kusimamia utendaji kazi wa mashirika na taasisi zilizopo chini ya Ofisi ya Rais TAMISEMI.