Habari

SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA LAFANYIWA UKAGUZI WA KIMENEJIMENTI


SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA LAFANYIWA UKAGUZI WA KIMENEJIMENTI

 Kibaha – 24, Novemba,2O15

Shirika la Elimu ni Miongoni mwa Taasisi zilizo chini ya usimamizi wa Msajili wa hazina zinazofanyiwa ukaguzi wa kimenejimenti,hayo yameelezwa na Kaimu Msajili wa Hazina Bw. Mwakibinga ,wakati akiongea na Menejimenti ya Shirika la Elimu jana katika ukumbi wa mikutano wa Shirika.

Akifafanua lengo la ukaguzi huo Bw. Mwakibinga amesema kuwa Ofisi ya Msajili wa Hazina ndiyo msimamizi wa rasilimali na vitega uchumi vyote vya Mashirika ya Umma  na makampuni ambayo serikali ina hisa kwa niaba ya Rais hivyo kwa kuzingatia wajibu wake inampasa kufanya ukaguzi wa kimenejimenti.

Alitaja maeneo ambayo uhakiki utafanyika ni pamoja na kuangalia wafanyakazi waliopo, uongozi,Bodi jinsi inavyosimamia  Sera za Serikali zinavyotekelezwa, kuangalia miongozo iliyopo,kuangalia kama vikao vinafanyika, mapato na matumizi na masuala yote yahusuyo uendashaji wa taasisi.

Aidha alifafanua kwa ujumla wanaangalia taasisi zote zilizo chini ya Msajili wa Hazina jinsi zinavyofanya kazi,kubainisha changamoto na kutafuta sulihisho mapema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Dkt. Cyprian Mpemba alishukuru ujio wa Kaimu Msajili wa Hazina Bw.Mwakibinga  na kwamba ujumbe ulioteuliwa kufanya ukaguzi wa kimenejimenti umekuja wakati muafaka kwani Shirika la Elimu Kibaha lina changamoto ambazo zinahitaji sulihisho la pamoja.