Habari

​Shirika la Elimu Kibaha lapokea msaada wa nyaya za uzio kutoka KEC SACCOS


Shirika la Elimu Kibaha (KEC) leo Jumatano tarehe 01/11/2023 limepokea msaada wa nyaya za kuweka uzio ‘roller’ 15 zenye thamani ya shilingi 1,650,000 kutoka Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Shirika la Elimu Kibaha (KEC SACCOS) kwa ajili ya kuweka uzio katika mabweni ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Kibaha.

Msaada huo umetolewa na Mwenyekiti wa bodi ya KEC SACCOS, Bw. Sixbert Luziga kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Bi. Chiku Wahady ambaye ameupokea kwa niaba ya Menejimenti ya Shirika hilo.

“Lengo la KEC Saccos ni kurudisha kwa jamii sehemu ya faida tunayoipata, tumeamua kutoa nyaya za kujengea uzio ili watoto wetu wanaokaa bweni wapate usalama kwao na vifaa vyao. Tumefurahi kutoa msaada huu, ni wajibu wetu kurudisha kwa jamii,” amesema Bw. Luziga.

Bi. Wahady amewashukuru KEC SACCOS kwa kutoa msaada huo kwa shule hiyo ambayo ipo chini ya Shirika la Elimu Kibaha na ametoa wito kwa SACCOSS nyingine kutoa msaada kwa jamii ikiwa ni njia ya kurudisha sehemu ya faida wanayoipata.

Pia, Meneja wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Shirika la Elimu Kibaha (KEC SACCOS), Bw. Emmanuel Mbuhe ametumia nafasi hiyo kuwaomba watumishi wa Serikali ambao hawajajiunga na chama hicho, wajiunge ili kuongeza nguvu na kufanikisha malengo ya kiuchumi na kijamii.

Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Wasichana Kibaha, Bi. Felista Mathias ameshukuru kwa kupatiwa msaada huo na kuomba wadau wengine wajitokeze kusaidia shule hiyo.

Akitoa shukurani kwa niaba ya wanafunzi wa shule hiyo, mwanafunzi Esther Mwasonoka ameushukuru uongozi wa KEC SACCOS kwa kuwapatia msaada kwa kuwa nguo na vifaa vingine wanavyotumia wakati wa kusoma vitakuwa katika hali ya usalama na kuwafanya wasome bila wasiwasi wa kuibiwa.