Habari

​Shirika la Elimu Kibaha lavuka malengo utoaji wa elimu ya ujuzi kupitia mtandao


Mradi wa kuwezesha na kuimarisha utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kwa njia ya mtandao leo Ijumaa tarehe 02/12/2022 umehitimishwa kwa mahafali ya kuhitimu mafunzo hayo na jumla ya wahitimu 6,157 wametunukiwa vyeti.

Akitoa taarifa ya mradi, Mratibu wa Mradi huo wa mafunzo ya ujuzi kwa njia ya mtandao uliofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa juhudi za Serikali ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Rogers Shemwelekwa ameeleza kuwa mradi huo umeonesha mafanikio makubwa sana kwa kuwa umetimiza malengo yake kwa ufanisi.

“Mradi huu, ulianza kama andiko maalumu kwenda Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) na baada ya maandiko hayo kushindanishwa, Shirika la Elimu Kibaha (KEC) likawa moja ya taasisi saba zilizoshinda na kupatiwa ruzuku ya Tsh. 131,220,000 kwa ajili ya kuandaa miundombinu ya kufundishia, kuwajengea uwezo wakufunzi na kutoa elimu kwa njia ya mtandao kwa wanufaika. Mradi ulianza rasmi tarehe 29/08/2022 na kukamilika tarehe 30/11/2022,” alisema Dkt. Shemwelekwa.

“Lengo la mradi lilikuwa ni kunufaisha Watanzania 300, lakini tuna jumla ya wanufaika 6,157 kati yao 221 wanatoka Tanzania visiwani na 141 ni kundi maalum la vijana walioacha matumizi ya dawa za kulevya (waraibu) ambao waliamua kupata ujuzi wa aina mbalimbali. Wanufaika wa mafunzo haya wamepatiwa mafunzo kwa nadharia na vitendo, ambapo wakufunzi walitoa mada mbalimbali, majaribio na mazoezi,” alisema Dkt. Shemwelekwa.

Akipongeza utekelezaji wa mradi huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa mahafali hayo, amelitaka Shirika la Elimu Kibaha kuwa na mpango endelevu kwenye uendeshaji wa mafunzo hayo kwa kuwa yana tija kubwa kwa jamii.

“Nawapongeza kwa kufanikiwa kutoa mafunzo kwa njia ya Mtandao kwa wanafunzi 6,157, mradi ambao umefadhiliwa na Benki ya Dunia kwa juhudi za Serikali ili kuwawezesha wananchi kupata ujuzi katika nyanja mbalimbali kwa njia ya elimu ya masafa. Kwa upande wa Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuwekeza kwa kiasi kikubwa hususani katika Vyuo vya Ufundi na Vyuo vya Maendeleo ya wananchi ili kutoa mafunzo bora,” alisema Prof. Shemdoe.

“Ndugu wahitimu huko muendako kalitumikieni Taifa, onyesheni uzalendo katika ujenzi wa Taifa letu. Shirikianeni na vijana wenzenu ambao hawakupata fursa ya kupata mafunzo kama haya.Kwa kufanya hivyo mtakuwa mmewarithisha ujuzi Watanzania wengine,” amesema Prof. Riziki Shemdoe

Mahafali haya ya 50 ya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha yalihusisha jumla ya wahitimu 6,318 waliopata mafunzo ya fani mbalimbali za ufundi bomba; ufundi wa umeme majumbani; ufundi wa magari; ufundi wa uungaji na uundaji vyuma; ufundi wa uwashi; ufundi wa useremala; ufundi wa ushonaji nguo na ubunifu wa mavazi; kilimo cha bustani na mazao mbalimbali; ufugaji; hotelia na udereva wakiwemo 6,157 wa mafunzo ya muda mfupi ya miezi mitatu kwa njia ya mtandao na 161 wa mafunzo ya muda mrefu ya miaka miwili chuoni hapo.