Habari
Shirika la Elimu Kibaha lazindua Dawati la Jinsia
Shirika la Elimu Kibaha (KEC) kupitia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha limezindua Dawati la Jinsia ili kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wa Chuo hicho endapo utajitokeza.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha, Bw. Anathe Nnko wakati akizindua Dawati hilo la Jinsia amesema, kazi ya Dawati hilo ni kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi wanaosoma katika Chuo hicho.
"Mwongozo wa Uanzishaji, Uendeshaji na Ufuatiliaji wa Dawati la Jinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu na Elimu ya Kati unatutaka tuanzishe Dawati la Jinsia ili tuzuie vitendo vya ukatili katika Chuo chetu cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha," amesema Bw. Nnko.
Bw. Nnko amesema makundi yanayofanya kazi ndani ya Shirika hilo yanapaswa kushirikiana na pamoja katika kuzuia vitendo vya kikatili.
Katika uzinduzi huo, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha, Bw. Joseph Nchimbi amesema Chuo hicho kimeunda Dawati la Jinsia ili kushughulikia na kuimarisha mfumo wa kutokomeza ukatili wa kijinsia.
"Chombo hiki muhimu kitakuwa kikipokea taarifa za ukatili na kufanya tathimini na kubuni mfumo rafiki na salama wa utoaji wa taarifa za ukatili," amefafanua Bw. Nchimbi.
Naye Mratibu wa Dawati la Jinsia, Bw. Fidel Maziku amewataka wanafunzi hao kutoa ushirikiano kwa wajumbe wa Dawati la Jinsia ili kutokomeza vitendo vya kikatili katika Chuo hicho endapo vitendo vya kikatili au unyanyasaji utajitokeza.
Wajumbe wa Dawati la Jinsia kwa upande wa walimu ni Bw. Redemptus Shoto, Bw. Konrad Muhuro, Bi. Agness Lulandala, Bi. Neema Msovu na upande wa wanafunzi wajumbe ni Mohamed Chuma na Naima Ramadhani.
Ukatili wa kijinsia ni kitendo chochote anachofanyiwa mtu au watu ambacho kinaweza kusababisha madhara ya kimwili, kiakili, kisaikolojia au mateso mengine.