Habari
Shirika, Sweden na Halmashauri watekeleza mradi wa jinsia
Shirika la Elimu Kibaha (KEC), Halmashauri ya Mji wa Kibaha na Wisbygymnsiet ya Manispaa ya Gotland nchini Sweden wamekutana na kupima uelewa wa jamii juu ya maswala ya kijinsia ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa usawa wa jinsia na malengo ya maendeleo endelevu 2030 (Sustainable Development Goals 2030).
Upimaji huo umefanywa kwa kuwahoji wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa jamii, wanafunzi na wananchi.
Akizungumza wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo, mratibu wa mradi huo kutoka Shirika la Elimu Kibaha Bi. Hildegarda Saudar amesema kuwa mradi wa usawa wa kijinsia unalenga kuongeza idadi ya wanawake katika ngazi ya maamuzi.
Pia, amebainisha kuwa mradi wa malengo ya maendeleo endelevu 2030 umelenga kutoa elimu kwa walimu na wanafunzi ili kuwa na uelewa pamoja katika utekelezaji wa miradi hiyo.
“Mradi wa malengo ya maendeleo endelevu umelenga kuwajengea uwezo walimu ambao watawafundisha wanafunzi madarasani kuhusu malengo ya maendeleo endelevu 2030 pamoja na usawa wa jinsia,” amesema Bi. Hildegarda.