WATUMISHI WA HALMASHAURI YA MANISPAA YA KIBAHA WATEMBELEA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA KUJIFUNZA USIMAMIZI WA MAKTABA.

Kibaha, Pwani Septemba 2025
Watumishi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wametembelea Shirika la Elimu Kibaha kwa ziara ya mafunzo kuhusu masuala ya uendeshaji wa maktaba, lengo likiwa ni kuboresha huduma za maktaba katika maeneo yao ya kazi.
Katika ziara hiyo, watumishi hao walipata fursa ya kujifunza kutoka kwa Bw. Silvanus Nyoni, mtaalamu wa maktaba wa Shirika la Elimu Kibaha, ambaye aliwaeleza kwa kina taratibu za usimamizi wa maktaba, uandikishaji wa vitabu, matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma, na usomaji kwa jamii.
Bw. Nyoni alisisitiza umuhimu wa maktaba kama kitovu cha maarifa na chombo muhimu cha kuhamasisha usomaji, hasa kwa vijana na wanafunzi.
Watumishi hao walionesha kufurahishwa na mafunzo hayo na walieleza kuwa yamewapa uelewa mpya wa jinsi ya kuboresha huduma za maktaba katika Manispaa ya Kibaha.
Ziara hii ni sehemu ya juhudi za kubadilishana uzoefu na kuboresha huduma kwa wananchi kupitia elimu endelevu kwa watumishi wa umma.
Maktaba ya Umma Kibaha, ni Maktaba kubwa pekee katika Mkoa wa Pwani ambayo inahudumia wakazi wa Mkoa wa Pwani na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam.