Habari

MKURUGENZI MTENDAJI WA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA DK. CYPRIAN MPEMBA AKABIDHI CHOO CHENYE THAMANI YA SHILINGI MILIONI 45 KWA UONGOZI WA SHULE YA MSINGI TUMBI


Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Elimu Kibaha Dk. Cyprian Mpemba leo amekabidhi choo kwa uongozi wa Shule ya Msingi Tumbi. Akikabidhi choo hicho kilichojengwa kwa thamani ya shilingi milioni 45 za Kitanzania, Dk. Mpemba amesema kuwa anafaraja kubwa kukabidhi choo  ambacho kilikuwa ni hitaji kubwa kwa shule hiyo.

Aidha Dk Mpemba amesema ameyafanyia kazi maombi ya uongozi wa Shule hiyo ya kujengewa choo  kipya baada ya  choo cha zamani  kuwa chakavu. Amesisitiza kuwa fedha ni chache za kukidhi mahitaji katika maeneo yote hivyo mfumo wa (ppp), yaani ushirikiano baina ya wadau wa maendeleo na serikali unafaa sana katika kuendelea kuchochea maendeleo. Ameitaka kamati ya Shule ijitahidi kupata fedha za kuweza kutekeleza miradi kama ya ukarabati wa Shule na Serikali itaungana nao katika juhudi hizo.

Awali akishukuru   Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Tumbi Bw. Jani Moses amesema ujenzi wa choo hicho  cha kisasa umeleta faraja kubwa kwa wanafunzi kwani watapata huduma katika choo bora. Pia alimuomba mkurugenzi asaidie kukarabati madarasa na  choo cha zamani  ili kiweze kutumika pia.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya shule ya Msingi Tumbi Bw.Hamisi Mbonde amemshukuru Mkurugenzi kwa kujenga choo cha kisasa. Ametaka wanafunzi waelimishwe namna bora ya kutumia choo hicho.

Shule ya Msingi Tumbi ni moja ya Shule za Msingi  za Wilaya ya Kibaha inayosifiwa kwa kutoa elimu bora.