Habari

Ujerumani, Serbia, Ethopia, Uganda wavutiwa na uanzishwaji wa FDC Tanzania


Shirika la Elimu Kibaha (KEC) leo Ijumaa tarehe 16/09/2022 wamekuwa wenyeji wa warsha ya wadau wa elimu kutoka nchi za Uganda, Ethiopia, Ujerumani, Serbia na Tanzania kwa ajili ya kujifunza jinsi ya uanzishaji na uendeshaji wa vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDC).

Warsha hiyo iliyodhaminiwa na Taasisi inayoshughulikia elimu ya watu wazima duniani (DVV) kwa kushirikiana na Taasisi ya Karibu Tanzania (KTO) pamoja na Shirika la Elimu Kibaha imelenga kujadili mafanikio ya uendeshaji wa vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDC) ili waweze kuanzisha kwenye nchi zao.

Akiwakaribisha katika warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Bw. Robert Shilingi, amewashukuru wadau hao kwa kulichagua Shirika la Elimu Kibaha kuwa mwenyeji wa warsha hiyo.

"Nachukua nafasi hii kuwashukuru kwa heshima kubwa mliyotupatia Shirika la Elimu Kibaha kuwa wenyeji wa warsha hii." Alisema Bw. Shilingi.

Pia Mkurugenzi wa taasisi inayoshughulikia elimu ya watu wazima duniani (DVV) Bw. Christoph Jost ameeleza kuwa taasisi yake inafanya kazi pamoja na wadau mbalimbali kwa manufaa ya jamii ili kukuza elimu ya watu wazima, kwa kuwapa watu maisha bora kupitia elimu wanayoipata kwenye vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDC).

"Kwa Tanzania, wanafunzi wa kike waliositisha masomo kwa sababu ya ujauzito, wanaruhusiwa kurudi shule baada ya kujifungua, hivyo wanapewa nafasi ya kuchagua mfumo wa kujipatia elimu hiyo iwe ni mfumo rasmi (kupitia shule za Serikali) au mfumo usio rasmi (kupitia vyuo vya maendeleo ya wananchi) ili kuendelea kutimiza ndoto zao." Alisema Bw. Jost.

Wadau hao walipata uzoefu wa uanzishaji na uendeshaji wa FDC kutoka kwa wakuu wa vyuo vya maendeleo ya wananchi vya Kibaha, Newala na Kisarawe.

Akibadilishana uzoefu na washiriki wa warsha hiyo, mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya wananchi Kibaha (KFDC), Bw. Joseph Nchimbi ameeleza kuwa, chuo hicho ni kikongwe, mwaka 1964 kilianzishwa kama kituo cha mafunzo kwa wakulima na 1965 kikabadilishwa na kuwa chuo cha maendeleo ya wananchi.

"KFDC imeanzishwa ili kukabiliana na umasikini kwa njia ya kutoa elimu kwa jamii kupitia kozi mbalimbali ambazo chuo inazitoa. Chuo kinafundisha kozi ndefu (kwa muda wa miaka miwili), kozi fupi (kwa muda wa miezi miwili mpaka sita) na elimu kwa njia ya mtandao. Chuo hiki kinatoa nafasi kwa wahitaji mbalimbali wakiwemo wenye mahitaji maalum ambao wanapewa nafasi kumi kila mwaka."

Akielezea namna vyuo vya FDC vinavyotoa elimu, Mkuu wa Chuo Cha Maendeleo ya wananchi Newala, Bw. Godfrey Nchimbi ameeleza kuwa vyuo hivyo vimeanzisha programu mbalimbali zinazowafanya wanafunzi kujifunza kwa urahisi na kuweka mazingira rafiki zikiwemo elimu za sekondari kwa mfumo usio rasmi, elimu za ujuzi, elimu ya watoto wadogo na programu ya kutumia michezo inayoitwa mpira fursa ili kuwavutia wanafunzi hasa mabinti kupenda mazingira ya kujifunzia.

Pia, Mkurugenzi wa Taasisi ya Karibu Tanzania (KTO) Bw. Maggid Mjengwa kupitia taasisi yake ameahidi kukiunganisha chuo cha maendeleo ya wananchi Kibaha (KFDC) kwenye programu ya kutoa elimu kwa mabinti waliopata ujauzito na kusitisha masomo ambao wanarudi kusoma tena baada ya kujifungua , ili kuikomboa jamii yetu na kuleta maendeleo.

Mfumo wa uendeshaji wa vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDC) upo katika nchi tano tu duniani ambazo ni Norway, Sweden, Denmark, Finland na Tanzani, ambapo Tanzania ni nchi pekee kwa bara la Afrika.

Warsha hiyo ya siku moja pia imehudhuriwa na Afisa Programu kutoka taasisi ya Elimu Haina Mwisho Bi. Angel Owusu; Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia vyuo vya maendeleo ya wananchi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bi. Magreth Musai; Mkurugenzi msaidizi anayeshughulikia elimu ya watu wazima kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bi. Godliver Mkala, wawakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Pwani, ofisi ya mkuu wa Wilaya ya Kibaha, watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha, na wanafunzi wa chuo cha maendeleo ya wananchi Kibaha.