Habari

‘Usawa wa jinsia utumike kuleta maendeleo endelevu Kibaha’


Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhe. Selina Msenga leo Jumanne tarehe 08/11/2022 amefungua kongamano la Sera ya Jinsia liliowahusisha wadau kutoka Shirika la Elimu Kibaha, Halmashauri ya Mji Kibaha na Manispaa ya Gotland nchini Sweeden, lililofanyika katika ukumbi wa Bertil Mellin uliopo Shirika la Elimu Kibaha.

Akifungua kongamano hilo, Mhe. Msonga amewataka washiriki wa kongamano hilo kushiriki kikamilifu katika kusikiliza mada zinazowasilishwa na kutoa michango ya mawazo yao katika utekelezaji wa Sera hiyo ya Jinsia kwenye maeneo yao ya kazi ili kuleta maendeleo kwa jamii wanayoisimamia na taifa kwa ujumla.

“Tuko hapa kwa sababu kubwa moja, tunahitaji sisi sote kufikia malengo ya usawa wa jinsia. Nchi yetu ni moja kati ya nchi wanachama wa Umoja wa Kimataifa ambazo zinatekeleza malengo ya maendeleo endelevu. Leo tupo hapa kwa ajili ya lengo namba 5 linalozungumzia usawa wa jinsia.” Amesema Mhe. Msonga.

“Kongamano hili linatusaidia kujenga uelewa juu ya usawa wa jinsia kwa nyinyi viongozi, ili nanyi muweze kupeleka elimu hii kwa wananchi wetu, ili kuleta urahisi katika kuhakikisha tunafikia malengo ya usawa wa jinsia. Yale ambayo tunayajua, tutaongeza ujuzi kutoka kwa wenzetu, yale ambayo hatuyajui tutapata nafasi ya kuuliza maswali na kuongeza uelewa.” Amesema Mhe. Msonga.

Akitoa mada katika kongamano hilo, Afisa maendeleo ya jamii, Halmashauri ya Mji Kibaha Bi. Anitha Lyoka, ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha malengo ya usawa wa kijinsia yanafikiwa imefanya jitihada mbalimbali zikiwemo uanzishwaji wa Sera ya jinsia ya mwaka 2000; uwepo wa katiba inayoruhusu upenyezaji wa masuala ya jinsia na uwezeshaji wa wanawake; uanzishwaji wa mifuko ya uwezeshaji wanawake kifedha; uwepo wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yanayojihusisha na masuala ya jinsia; na uanzishwaji wa madawati ya jinsia katika polisi, ofisi za Miji na Wilaya.

Akiwasilisha hali halisi ya utekelezaji wa usawa wa jinsia nchini Sweeden, Bi. Marita Vesterlund ameeleza kuwa usawa huo unazingatia katika sheria zao kwa maeneo yote yakiwemo upatikanaji wa ajira, malipo kwa wasio na ajira na upatikanaji wa huduma za kijamii.

Muwasilishaji mada wa pili katika kongamano hilo, Bw. Gaudence Nyamwihura ameeleza kuwa Sera ya Maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000 lengo lake ni kuingiza dhana ya jinsia na kuangalia usawa kati ya wanawake na wanaume kwa sababu Tanzania inaamini kuwa ukosefu wa usawa wa kijinsia unaondoa upatikanaji wa maendeleo endelevu.

Kongamano hilo la siku mbili kuanzia tarehe 08 hadi 09/11/2022 linalofanyika katika ukumbi wa Bertil Mellin uliopo Shirika la Elimu Kibaha limehudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC)Bw. Robert Shilingi; wawakilishi kutoka Manispaa ya Gotland – Sweeden; watumishi wa KEC; wenyeviti na watendaji wa Serikali za mitaa za Mji wa Kibaha; wajumbe wa mabaraza ya wawezeshaji wanawake kiuchumi; wajumbe wa dawati la jinsia KEC; na watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Hii ni moja ya njia za kufanikisha mkakati wa utekelezaji wa mradi wa pamoja kuelekea maendeleo endelevu 2030 ambao Shirika la Elimu Kibaha, Halmashauri ya Mji Kibaha na Manispaa ya Gotland-Sweeden wanatekeleza ikiwa ni njia ya kudumisha ushirikiano wao.