Habari

WAFANYAKAZI BORA WA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA WAPATIWA VYETI VYA UTUMISHI BORA SERIKALINI


WAFANYAKAZI BORA WA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA WAPATIWA VYETI VYA UTUMISHI BORA SERIKALINI

Tarehe 12 Juni,2017

Wafanyakazi bora wa Shirika la Elimu Kibaha leo wamekabidhiwa vyeti vya utumishi bora Serikalini. Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika Ukumbi wa B. Merlin.

Awali akiwapongeza wafanyakazi hao kabla ya kuwakabidhi vyeti, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha Bw. Robert Shilingi amewapongeza wafanyakzi hao kwa kuwa ni wafanyakazi  bora na amewataka  waendelee kuongeza juhudi katika kazi.

Pia amevipongeza vyama vya wafanyakazi vilivyopo katika Shirika la Elimu Kibaha ambayo ni CWT, TUGHE NA CHODAWU mwaka huu vimeshauri namna bora ya kushiriki katika sherehe za wafanyakazi mwaka 2017 ambapo wafanyakazi wengi zaidi waliweza kushiriki katika Sherehe za Mei Mosi kimkoa zilizofanyika Wilayani Bagamoyo.

Amelipongeza Baraza la Wafanyakazi ambalo limeshauri kuwe na hafla fupi ya kuwakabidhi vyeti wafanyakazi hodari na kwamba anaamini Baraza hilo litaendelea kutoa ushirikiano katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Shirika la Elimu Kibaha.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi la Shirika la Elimu Kibaha Bw. Alexander Kashaija aliwapongeza wafanyakazi wote bora na amewaomba waendelee kutoa huduma bora kazini.

Akishukuru kwa niaba ya wafanyakazi hodari waliokabidhiwa vyeti Bw. Joseph Kibindu ameshukuru Menejimenti na Baraza la Wafanyakazi kwa kuwa pamoja   na changamoto zilizopo wametoa  zawadi kwa watumishi hodari kwa wakati. Alisema wao kama wafanyakazi hodari wa Shirika wataendelea kuafanya kazi kwa maslahi ya Shirika. Shirika la Elimu Kibaha limekuwa na desturi ya kuwatunuku zawadi na vyeti kwa wafanyakazi hodari kila mwaka.