Habari

​Wahitimu Chuo cha Afya watakiwa kujali afya kuliko maslahi binafsi


Wahitimu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Kibaha (KCOHAS) leo Ijumaa tarehe 28/07/2023 wametakiwa kujali afya za wagonjwa kuliko maslahi yao binafsi.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Bw. Adolf Ndunguru akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 56 ya KCOHAS yaliyofanyika katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha (KEC).

“Wito wangu kwenu popote mtakapokwenda toeni huduma bora. Kipaumbele kiwe kwanza kutoa huduma na siyo maslahi ya fedha. Kumbukeni kuwa uhai wa binadamu ni tunu ya mwenyezi Mungu, haiwezi kufidiwa na kitu chochote. Itikieni wito huu kwa unyenyekevu mkubwa, jiepusheni na lugha zisizofaa kwa watu mtakaowahudumia,” amesema Bw. Ndunguru.

Wakati huo huo Bw. Nunguru amepongeza Shirika la Elimu Kibaha kwa kutenga hekari 100 za upanuzi wa chuo cha KCOHAS na kuahidi OR-TAMISEMI itasaidia kutafuta fedha za ujenzi wa majengo mapya ili Chuo hicho kidahili wanafunzi wengi zaidi na kuwezesha kutoa idadi kubwa ya wataalamu wa afya.

“Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imelipa umuhimu suala la kuimarisha sekta ya elimu na afya nchini na OR-TAMISEMI tumepewa dhamana hiyo hivyo tutafanya kila linalowezekana kutafuta rasilimali fedha ili kuboresha na kuongeza miundombinu ya kujifunzia na kufundishia hivyo kuakisi umuhimu wa chuo hiki," amesema Bw. Ndunguru.

Mahafali hayo yamehusisha wahitimu 199 wa stashahada wakiwemo 93 wa fani ya uuguzi na ukunga, na 106 wa fani ya utabibu ambao wanatarajiwa kwenda kutoa huduma hiyo kwa wananchi ikiwa ni lengo mojawapo la uanzishwaji wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) ambapo mwanzilishi Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere alilenga kupambana na maadui watatu wa maendeleo ambao ni umasikini, ujinga na maradhi kwa njia ya elimu.