Habari

Wahitimu wa Mahafali ya 51 KFDC watakiwa kujiajiri


Wahitimu 171 wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Kibaha kilichopo chini ya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) wametakiwa kutumia ujuzi walioupata chuoni hapo kujiajiri kwa kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali vilivyopo maeneo yao ya makazi.

Hayo yamesemwa Alhamisi tarehe 16/11/2023 na Mhe. Mussa Ndomba, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha, akiwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, akimwakilisha Mhe. Sylivestry Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini.

Njia rahisi ya kufanikiwa katika Maisha yenu ni kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali. Humo mtapata fursa ya kuunganisha nguvu zenu, ujuzi na kutumia rasilimali zinazopatikana katika maeneo yenu. Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mama yetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipambanua vizuri kuimarisha Uchumi, Sera nzuri za Kibenki, ukopeshaji na ushirika wa akiba na mikopo, vijana wangu tumieni fursa hiyo, amesema Mhe. Ndomba.

Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wenzake, Asha Njowoka, Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa KFDC, ameeleza kuwa elimu waliyoipata chuoni hapo itawasaidia kujiajiri, kuajiriwa na kuajiri.

Chuo kimetusaidia kupata ujuzi wa kutosha kwa fani tulizosoma na hata ujuzi tofauti na fani tunazosoma, hivyo tunaamini tutaweza kujiajiri, kuajiriwa na kuajiri,” amesema Asha Njowoka.

Pia, Mkuu wa Chuo cha KFDC, Bw. Joseph Nchimbi, alitoa taarifa fupi ya wahitimu kuwa walianza mafunzo yao Januari 2022, wanahitimu wakiwa 171, kati yao wanawake 70 na wanaume 101 kwenye fani za ufundi bomba, ufumdi umeme, ufundi magari, upishi, mifugo, uundaji na uungaji wa vyuma, ubunifu wa mitindo na ushonaji, kilimo, ufundi uashi na useremala. Mafunzo hayo yanalenga kumpatia mwanachuo ufundi stadi unaomuwezesha kupambana na mazingira yake.

Mahafali hayo ya 51 pia yalihudhuriwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibaha, Bi. Mwajuma Nyamka, Mwenyekiti wa Vijana CCM Kibaha Mji, Bw. Ramadhan Kazembe, viongozi wa dini, watumishi walimu na wasio walimu wa Chuo cha KFDC, wazazi na walezi wa wahitimu hao na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Elimu Kibaha na wajumbe wake wa timu ya Menejimenti ya Shirika hilo.