Habari

WAKULIMA WAPATIWA MAFUNZO ILI WAWEZE KUFAIDIKA KIUCHUMI KUPITIA KAMPUNI YA ORGANIA


WAKULIMA WAPATIWA MAFUNZO ILI WAWEZE KUFAIDIKA KIUCHUMI KUPITIA KAMPUNI YA ORGANIA

Kibaha – 1, Desemba ,2O15

Wakulima kutoka Kibaha na Kisarawe leo wamepatiwa mafunzo ya namna bora ya kulima na kunufaika kwa kuiuzia mazao Kampuni ya Uzalishaji kuku wa kisasa ya  Organia. Mafunzo hayo yamefunguliwa rasmi na Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Pwani Eng. Evarist Ndikilo.

Akifungua mafunzo hayo Mhe. Ndikilo amesema kuwa baada ya kupata maelezo kuhusu nia ya Kampuni ya Organia kushirikisha wakulima katika kuuza mazao kwao ,ameridhika kuwa mradi huo unalenga kupambana na umasikini.

Alifafanua kitendo cha wakulima kupatiwa mafunzo ya namna bora ya kuongeza uzalishaji kwa kiwango cha kimataifa kitawawezesha kupata ajira,kuongeza kipato na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja . Pia  amesema kuwa anaamini mradi  huo wa ufugaji kuku utaiwezesha Serikali kupata kodi itakayolipwa na kampuni hiyo.

Akitambulisha mradi huo wa wakulima na wafugaji kushiriki katika uzalishaji wa mazao yatakayouzwa kwa Kampuni ya Organia Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la Elimu Kibaha Dkt. Cyprian Mpemba amesema hii ni fursa nzuri kwa wakulima ,hivyo ni vyema wakasikiliza mafunzo hayo na kuona ni jinsi gani watayatumia kuweza Kujiongezea kipato.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kampuni ya Organia Bw. Tahir amesema kwamba mradi huo unategemewa  kunufaisha pande zote mbili, mazao yatakayozalishwa yatakuwa yenye ubora wa hali ya juu, mazingira ya biashara yatakuwa mazuri na kwamba hii itawezesha wakulima kupata faida na  hivyo kukua kiuchumi.

Kampuni ya Organia iliingia mkataba na Shrika la Elimu Kibaha Februari 2014 kwa ajili ya kuzalisha kuku wa kisasa ambapo  wakulima na wafugaji watanufaika kwa kufanya biashara na  kampuni hiyo. Mradi huo  utawahusisha wakulima na wafugaji katika   ufugaji wa kuku bora,uzalishaji wa chakula kama vile  soja , mahindi meupe na njano pia  kuhifadhi kuku  kuuza na  kuongeza kipato.